Michezo

Matteo Darmian avunja ndoa na Parma na kuingia kambini mwa Inter Milan

October 5th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

MWANASOKA wa zamani wa Manchester United, Matteo Darmian, amejiunga na kikosi cha Inter Milan kwa mkopo wa mwaka mmoja kutoka Parma.

Kwa mujibu wa maafikiano, Inter watakuwa huru kumpokeza beki huyo mkataba wa kudumu mwishoni mwa kipindi chake cha mkopo.

Darmian ambaye ni raia wa Italia, alichezea Parma katika jumla ya mechi 34 msimu uliopita wa 2019-20 baada ya kuingia katika sajili rasmi ya kikosi hicho kwa mkataba wa miaka minne akitokea Man-United mnamo Septemba 2019.

Kwa kujiunga na Inter ya kocha Antonio Conte, Darmian anaungana sasa na waliokuwa wanasoka wenzake kambini mwa Man-United – Ashley Young, Romelu Lukaku na Alexis Sanchez.

Sogora huyo mwenye umri wa miaka 30 alianza kusakata soka ya kitaaluma akivalia jezi za watani wa tangu jadi wa Inter katika Ligi Kuu ya Italia (Serie A), AC Milan.