Habari Mseto

Matukio 2019: Mafuriko yaligeuka fursa ya kipato kwa baadhi ya vijana Mwiki

December 31st, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

NAIROBI ni miongoni mwa kaunti zilizoathirika na mvua iliyopitiliza iliyoshuhudiwa mwishoni mwa mwaka 2019.

Ingawa imepungua Nairobi na kaunti jirani, kuna maeneo yanayoendelea kushuhudia mvua hiyo ya gharika.

Wakati wa mvua, baadhi ya wakazi hasa wanaofanya kazi jijini Nairobi walijipata kuhangaika kusafiri kwa ajili ya barabara kufurika maji.

Mwiki ni baadhi ya mitaa ambayo shughuli za usafiri na uchukuzi zilikuwa kisunzi. Wanaotumia kivuko cha daraja linalounganisha eneo la Maguo lililoko kaunti ya Kiambu na Mwiki, walikuwa na wakati mgumu kusafiri. Kivuko hicho kimejengwa katika mto unaogawanya Kiambu na Nairobi.

Aidha, daraja hilo lilifurika kiasi cha watumizi kushindwa kuvuka kwa miguu. Mahangaiko hayo yakishuhudiwa, kundi la vijana lilipata mwanya wa kujizolea mapato kwa kuvusha watu.

“Tunatoza Sh20 pekee kuvusha mtu mmoja kwa mkokoteni,” akasema Lawrence Kariuki, mmoja wa kundi hilo. Kijigari hicho kinachosukumwa kilikuwa kikipakiwa kadri ya watu sita.

Kwa kuvua viatu, kundi la vijana hao wapatao wanne walikuwa wakisukuma mkokoteni, wawili mbele na wawili kandokando (kwa mujibu wa picha tulizonasa wakati wa shughuli hiyo).

Vijana hao walisifia mvua iliyoshuhudiwa, wakihoji iliwapa kibarua cha muda. “Hatuna kazi, tunategemea vibarua vinavyojiri kama hivi kusaidia wananchi kwa mkokoteni,” akasema kijana mwingine wa kundi hilo.

Jane Wanja, mfanyabiashara Mwiki na anayeendea bidhaa Kiambu alilalamikia hali mbovu ya miundomsingi kama barabara.

“Mvua inaponyesha hususan ya mafuriko, daraja tunalotumia huwa hatari,” Wanja akaambia ‘Taifa Leo’ wakati wa mahojiano.

Ni katika msimu wa mvua hiyo ambapo baadhi ya sehemu Thika Superhighway zilifurika maji, wenye magari wakilazimika kusubiri mvua kupungua.

Sawa na Mwiki, wakazi wa baadhi ya maeneo Thika pia walikumbana na pandashuka hizo.

Daraja la Tola, Thika lilikuwa mojawapo yaliyovurika na kuwa hatari kwa wapita njia.

Kulingana na idara ya utabiri wa hali ya anga mvua hiyo ya gharika ilitabiriwa kuendelea hadi mwishoni mwa Desemba 2019.

Msimu wa sherehe za Krismasi, Kaunti ya Kisumu ilishuhudia mvua iliyopitiliza iliyosababisha mamia ya watu kuhama makwao kufuatia ongezeko la maji lililofunika nyumba zao. Maeneo yaliyoathirika pakubwa ni Kibos, Ogango, Lolwe, Nyamasaria, Pipeline, Buoye na Manyatta.

Zaidi ya watu 100 wameripotiwa kufa maji maeneo mbalimbali nchini.

Watu wanaonywa kupitia maeneo yaliyofurika hasa barabara na mito. Pia, si salama kusafiri wakati mvua inanyesha hususan katika maeneo yenye historia ya mafuriko.