Habari Mseto

MATUKIO 2019: Watu mashuhuri walioacha pengo baada ya kufariki

December 30th, 2019 6 min read

Na CECIL ODONGO

ZIKIWA zimesalia saa za kuhesabika tu kabla ya kuaga mwaka huu wa 2019, wapo viongozi maarufu wenye mchango muhimu katika mawanda mbalimbali ya maisha hapa Kenya na Afrika kwa jumla walioaga dunia.

Baadhi ya watu mashuhuri ambao nafsi zao zilionja uchungu wa mauti ni aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Safaricom Bob Collymore, Gavana wa Bomet Joyce Laboso, mwanasoka Joe Kadenge, mbunge wa Kibra Ken Okoth, Msanii na mfanyabiashara msanii Bruce Odhiambo, Mwanabima Karanja Kabage, mwanamuziki John De Mathew na mwanaspoti tajika Robert Ouko.

Kwenye dira ya Afrika, aliyekuwa Rais wa Zimbabwe aliyeondolewa mamlakani mnamo 2017 Robert Mugabe pia aliaga dunia nchini Singapore.

JOE KADENGE: Bw Kadenge alikuwa mwanasoka stadi enzi zake ambaye mchango wake kwa taifa hili hautawahi kusahaulika daima dawamu. Aling’aa katika kila mechi aliyochezea timu ya taifa Harambee Stars kuanzia miaka ya 70 hadi mwanzo wa miaka ya 80 alipostaafu soka.

Miaka hiyo kauli ‘Kadenge na mpira’ ilikuwa maarufu kwenye kinywa cha kila mtoto mdogo kutokana na jinsi watangazaji walivyomiminia sifa wakati wa kutangaza mechi za Harambee Stars dhidi ya wapinzani mbalimbali.

Hakika alikuwa mchezaji hodari ambaye aliwala wapinzani chenga za maudhi na kufunga mabao kwa njia ya ustadi mno.

Baadhi ya washikadau nchini pia wamemtaja kama nguli wa soka nchi na kudai kwamba hakuna katika kizazi cha sasa ambaye amefikia kiwango chake au kulinganishwa naye.

Zimwi la mauti lilimnyakua Bw Kadenge mnamo Julai 7, 2019 huku viongozi wakuu nchini wakiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta, Aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga na Naibu Rais William Ruto wakimsifu na kumtaja kama mzalendo kindakindaki.

BOB COLLYMORE: Bw Collymore alikuwa amehudumu kama Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya mawasiliano ya Safaricom kwa miaka 10 tangu uteuzi wake kwenye kwenye kampuni hiyo mnamo 2010.

Alisifiwa kwa kutekeleza mageuzi makubwa Safaricom na kuifanya kampuni bora zaidi nchini, iliyosifika sana duniani.

Mchango wake hasa ulisifiwa zaidi kutokana na kuimarika kwa huduma ya kutuma pesa kupitia simu za mkononi maarufu kama Mpesa kando na huduma nyinginezo ambazo zilifanya kampuni hiyo kupiku nyingine nchini na Afrika nzima.

Kifo chake mnamo Julai 1 baada ya kuugua kansa kwa muda mrefu kilizaa wingu la simanzi nchini, wengi wakimsifia kwa kujenga na kubadilisha safaricom pakubwa.Mwili wake ulichomwa katika eneo la kuchoma miili ya Kariokor mnamo Julai 2 kwenye hafla iliyoshuhudiwa na mkewe Wambui Kamiru na wanafamilia wengine.

KEN OKOTH: Wakazi wa eneobunge la Kibra walipigwa na butwaa kutokana na kifo cha Bw Okoth mnamo Julai 26, 2019. Alikuwa mbunge mchapakazi ambaye alikuwa ameugua saratani na hata kutafuta matibabu nje ya nchi kwa miezi kadhaa lakini baadaye akafa baada ya kulemewa sana na ndwele hiyo.

Bw Okoth alisifiwa sana na wakazi wa Kibra kutokana na jinsi alivyobadilisha maisha yao kupitia miradi ya maendeleo tangu achaguliwe kupitia chama cha ODM mnamo 2013.

Hata hivyo, kizazaa kilizingira mazishi yake baada ya diwani mteule wa bunge la kaunti ya Nairobi Ann Thumbi kudai alikuwa amejaaliwa mtoto na mbunge huyo.

Kilichozua maswali zaidi hasa ni hatua ya mkewe Monica Okoth kuongoza uchomaji wa mwili wake Kariokor huku mamake na wanafamilia wengi wakisusia mazishi hayo, wakitaka mwili huo uzikwe kulingana na tamaduni ya jamii za Waluo nyumbani kwao Kaunti ya Homa Bay.

JOYCE LABOSO: Gavana huyu wa Bomet pia alikuwa kati ya viongozi ambao ugonjwa wa kansa ulisababisha mauti yao ghafla na kuwashangaza Wakenya mno.

Aliaga dunia Julai 29, 2019 akiendelea kupata matibabu katika hosopitali ya Nairobi baada ya kuwa nje ya nchi kwa miezi kadhaa akitibiwa.

Ikizingatiwa alikuwa kati ya magavana watatu wanawake waliochaguliwa kwenye uchaguzi mkuu wa 2017, wakazi wa Bomet walikuwa na imani tele kwamba Bi Laboso ambaye kati ya 2008-hadi 2017 alikuwa mbunge wa Sotik, angewatimizia miradi mingi ya maendeleo jinsi alivyoahidi wakati wa kampeni.

Alizikwa nyumbani kwa mumewe Edwin Abonyo katika eneobunge la Muhoroni, Kaunti ya Kisumu mnamo Agosti 3 huku mumeme akiwasisimua waombolezaji kwa hotuba zake zilizojaa ucheshi na ufasaha kwenye ibada za mazishi zilizoandiliwa, Nairobi, Bomet na Muhoroni.

ROBERT MUGABE: RAIS huyo wa zamani wa Zimbabwe aliaga dunia mnamo Septemba 6 katika hospitali ya Gleneagles nchini Singapore.

Hii ni baada ya kuondolewa mamlakani na jeshi mnamo 2017 na Rais wa sasa Emmerson Mnangagwa kuchukua usukani baada ya uchaguzi mkuu mwaka wa 2018.

Rais Mugabe alizikwa nyumbani kwake katika kijiji cha Kutama Septemba 29, 2019 badala ya eneo lililotengwa kwa mazishi ya mashujaa jijini Harare.

MOHAMMED MORSI: Alikuwa Rais wa zamani wa Misri ambaye alipinduliwa na wanajeshi mwaka wa 2013 baada ya kuhudumu kwa mwaka mmoja pekee.

Morsi aliyefariki akiwa na umri wa miaka 67, ndiye alikuwa rais wa kwanza wa taifa hilo kuchaguliwa kidemokrasia.

Alishinda uchaguzi huo kwa sababu ya umaarufu wake katika uongozi wa kikundi cha Muslim Brotherhood ambacho baadaye kiliharamishwa.

Morsi alifariki kortini Juni wakati kesi ambapo alishtakiwa kwa madai ya ujasusi haramu dhidi ya taifa ilikuwa ikiendele

ZINE AL-ABIDINE BEN ALI: Alikuwa Rais wa zamani wa Tunisia ambaye utawala wake ulipinduliwa mwaka wa 2011 baada ya kuongoza kwa miaka 23.

Ali alifariki akiwa na umri wa miaka 83.

Mapinduzi yake yalikuwa ya kwanza kati ya mengine yaliyochipuka na kusambaa katika mataifa ya Kiarabu yaliyo ukanda wa Mashariki ya Kati.

Baada ya kupinduliwa, Ali alitorokea Saudi Arabia ambako alifariki Septemba.

JOHN DE’MATHEW: Alikuwa kati ya wanamuziki maarufu na shupavu kutoka eneo la Mlima Kenya aliyejizolea umaarufu mno kwa muda wa miaka 30.

Alijizolea sifa kutokana na uimbaji wake wa nyimbo zilizovutia raia na kukemea uongozi mbaya wa wanasiasa.

Viongozi kutoka ukanda wa Mlima Kenya pia walishabikia nyimbo zake na kuzitumia sana wakati wa kampeni za chaguzi mbalimbali.

Bw De’ Mathew aliaga dunia kwenye ajali mbaya ya barabarani mnamo Agosti 18, 2019 na akazikwa Agosti 24, 2019 katika eneobunge la Gatanga, Nyeri.

Mazishi yake ilihudhuriwa na Rais Uhuru Kenyatta, Naibu wake William Ruto, Kinara wa upinzani Raila Odinga miongoni mwa viongozi wengi mashuhuri kutoka Mlima Kenya na Bonde la Ufa.

BRUCE ODHIAMBO: Gwiji huyo wa kurekodi muziki ambaye alishiriki biashara mbalimbali aliaga dunia mnamo Januari 8, 2019.

Alikuwa rafiki mkubwa wa Rais Uhuru Kenyatta tangu enzi zao wakisoma katika shule ya upili ya St Mary’s jijini Nairobi.

KARANJA KABAGE: Alikuwa moja wa Wakenya ambao walifanikiwa sana katika ulingo wa biashara ya bima huku akiwa pia wakili tajika aliyeshamiri sana katika taaluma ya uanasheria.

Waliomwomboleza walimtaja kama mtu mwenye bidii ambaye alitangamana na raia wa kila tapo. Alifariki Julai 5, 2019 kwenye ajali katika barabara ya Southern by-pass, karibu na Kibra akielekea nyumbani kwake.

ROBERT OUKO: Robert Gwaro Ouko alikuwa kwenye timu iliyoshinda dhahabu kwenye mbio ya 4×400 katika michezo ya Olimpiki 1972 mjini Munich, Ujerumani.

Alikuwa kati ya wanariadha waliotesha mbegu ya umaarufu wa riadha nchini miongoni mwa watimkaji wa zamani na wale wa sasa.

OTIENO ODEK: WIKI mbili zilizopita, Jaji wa mahakama ya rufaa ya Kisumu Otieno Odek alipatikana ameaga dunia nyumbani kwake katika mtaa wa Milimani jijini Kisumu.

Marehemu ambaye alizikwa Ijumaa Disemba 27, iligunduliwa aliaga kutokana na kuganda kwa damu kwenye mguu wake huku waliohudhuria ibada ya kumuaga wakimsifu kama mtu mchapakazi ambaye alijitolea kuhudumia taifa hili.

Mazishi yake ilihudhuriwa na majaji na mahakimu kutoka idara ya mahakama wakiongozwa na Jaji Mkuu David Maraga na huku kiongozi wa ODM Raila Odinga akiwaongoza wanasiasa kumwomboleza mwendazake ambaye alikuwa na umri wa miaka 56.

CHARLES RUBIA: Mwanasiasa huyu wa upinzani aliyekuwa meya wa kwanza wa jiji la Nairobi alifariki mnamo Disemba 23, 2019.Bw Rubia pia anakumbukwa kwa kuhudumu katika serikali ya Rais wa kwanza Mzee Jomo Kenyatta na Rais Mstaafu Daniel Moi wakati huo pia akiwa mbunge wa Starehe. Marehemum hata hivyo alijizolea sifa kochokocho kwa kuongoza jitihada za kupigania mfumo wa vyama vingi pamoja na viongozi wengine kama Kenneth Matiba, Raila Odinga, Masinde Muliro, James Orengo, Jaramogi Oginga Odinga na viongozi wengine.Aliaga dunia hata kabla ya kushinda kesi ambayo alikuwa amewasilisha akiitaka serikali imlipe ridhaa kutokana na mateso aliyoyapokea akipigania kutokomezwa kwa enzi za chama kimoja.

FATUMA TABWARA: Bi Tabwara ambaye alikuwa Naibu Kamishna wa Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano(NCIC) aliaga dunia Jumapili Desemba 29 baada ya kuanguka akihudhuria harusi ya mtoto wa mmoja wa mwakilishi wadi Kaunti ya Kwale.

Juhudi za kuokoa maisha yake hazikufanikwa baada ya kifo chake kuthibitishwa alipofikishwa hospitalini.

Aliteuliwa kama kamishina wa Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano(NCIC) mnamo Oktoba 22 na Rais Uhuru Kenyatta kabla ya kuteuliwa naibu mwenyekiti wa tume hiyo Novemba 22 baada ya kuapishwa kwenye majengo ya mahakama ya juu na Jaji Mkuu David Maraga.

TIGER POWER (CONRAD NJERU KARUKENYA): Alikuwa jabali mwenye nguvu za ajabu mno na aliwahi kutoa wito kwa binadamu yeyote anayejiona ana nguvu nyingi amkabili.

Bw Power, 72 aliaga dunia siku ya pili ya mwaka huu(Januari 2, 2019) katika hospitali ya Kimisheni ya Consolata eneo la Kyeni, kaunti ya Embu. Cha ajabu ni kwamba Bw Power alikuwa na nguvu za kuvunja msumari na aliwahi kuvuta gari kubwa aina ya Land Cruiser kwa kutumia meno yake. Aliwahi kupokea tuzo ya Rais enzi za utawala wa Rais Mstaafu Mwai Kibaki japo aliaga dunia akiwa maskini sana na iliwahi kuripotiwa kwamba alishindwa kulipa bili ya kimatibabu ya Sh7,000.

BINYAVANGA WAINAINA: Alifahamika kimataifa kama mwandishi shupavu na mtetezi wa haki za wapenzi wa jinsia moja. Binyavanga alifariki Mei akiwa na umri wa miaka 48. Alikuwa mshindi wa tuzo la kifahari la uandishi la Caine Prize katika mwaka wa 2002. Aliwahi pia kutajwa miongoni mwa watu 100 wenye ushawishi mkubwa kimataifa na jarida mashuhuri la Time, kutokana na juhudi zake za kutetea haki za mashoga.