Habari za Kitaifa

Matulo kugeuzwa uwanja wa ndege wa kimataifa

June 1st, 2024 1 min read

NA SHABAN MAKOKHA

UWANJA mdogo wa ndege wa Matulo katika Kaunti ya Bungoma utafanyiwa maboresho kuwa uwanja wa kimataifa wa ndege, ametangaza Rais William Ruto.

Akihutubu katika uwanja wa Masinde Muliro Kanduyi kwenye sherehe za kitaifa za Madaraka Dei, Dkt Ruto alisema lengo ni uwanja huo kutumika na wenyeji wa Magharibi, Wakenya kutoka maeneo mengine, taifa jirani la Uganda na dunia nzima kwa ujumla.

Aliitaka serikali ya Kaunti ya Bungoma ikiongozwa na Gavana Kenneth Lusaka kushauriana na wakazi wanaoishi karibu na uwanja huo wa ndege ili kuwahamisha na kutoa nafasi ya upanuzi.

Awali uwanja huo mdogo wa ndege ulikuwa umetengewa zaidi ya ekari 70 za ardhi, lakini sehemu yake ndogo imevamiwa na umma.

“Ninamwagiza gavana wa Bungoma ashauriane na wakazi kwa nia ya kupata ardhi ya kutosha ili uwanja huo mdogo wa ndege uwe na nafasi ya kutosha ili kufanyiwa maboresho kuwa wa kiwango cha kimataifa ili kupiga jeki shughuli za kiuchumi,” akasema Dkt Ruto.

Alisema serikali ya kitaifa itatoa fedha kwa ajili ya upanuzi wa barabara inayotumika ndege zikipaa na kutua.

Pia aliahidi kufanya maboresho katika sehemu ya abiria wanaowasili na kuondoka.

Ujenzi wa uwanja mdogo wa ndege wa Matulo ulifanyika kama sehemu ya maandalizi ya sherehe za 61 za Madaraka Dei.

Ndege ya Rais ilitua katika uwanja huo alipofika Bungoma mnamo Mei 30, 2024, kuanza ziara yake ya siku nne ambayo itatamatika Jumapili.

Uwanja mdogo wa ndege wa Matulo katika Kaunti ya Bungoma. PICHA | JESSE CHENGE