Habari za Kitaifa

Matumaini deni la Kenya la Sh11 trilioni litapungua thamani ya shilingi ikianza kupanda

February 21st, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

DENI la Kenya liliongezeka kwa Sh1.93 trilioni kufikia Desemba mwaka uliopita, hali ambayo imefikisha deni hilo kuwa jumla ya Sh11.14 trilioni.

Kulingana na wataalamu wa masuala ya kiuchumi, hilo linamaanisha kuwa deni hilo lilikuwa likiongezeka kwa Sh5.29 bilioni kila siku mwaka wote wa 2023.

Ongezeko hilo limetajwa kuchangiwa na kushuka kwa thamani ya shilingi dhidi ya fedha za kigeni.

Mwaka uliopita pekee, shilingi ya Kenya ilipoteza thamani yake dhidi ya dola ya Amerika kwa asilimia 26.8.

Hali hiyo imetajwa kuchangia sana ongezeko la madeni hayo. Deni la nje liliongezeka kwa Sh1.4 trilioni, huku madeni ambayo serikali inadaiwa na taasisi za kifedha humu nchini yakiongezeka kwa Sh1.9 trilioni.

“Deni la Kenya kijumla liliongezeka kwa Sh1.93 trilioni kufikia Desemba 31, 2023 na kufikia Sh11.14 trilioni. Hilo ni ikilinganishwa na Sh9.2 trilioni kufikia Desemba 2022. Kiwango hicho kinajumuisha asilimia 54.7 ya deni la nje na Sh45.3 ya deni la taasisi za kifedha hapa nchini,” ikaeleza Wizara ya Fedha, kwenye ripoti ya kutathmini bajeti kati ya Oktoba na Desemba 2023.

“Ongezeko la deni la nchi limechangiwa na mikopo tunayoendelea kuchukua kutoka kwa taasisi za nje za kifedha; kubadilika kwa thamani ya shilingi ya Kenya kati ya masuala mengine,” ikaeleza ripoti hiyo.

Kutoka Januari hadi mwishoni mwa Desemba 2023, deni la jumla la nje liliongezeka kwa Sh1.4 trilioni na kufikia Sh6 trilioni.

Deni la ndani liliongezeka kwa Sh514.5 na kufikia Sh5 bilioni.

Hata hivyo, wadadisi wa masuala ya kiuchumi wanasema kuwa huenda mzigo wa madeni unaowakumba Wakenya ukaanza kupungua, baada ya thamani ya shilingi kuanza kupanda.

Wiki iliyopita, thamani ya shiligi ya Kenya dhidi ya dola iliimarika kutoka Sh160 hadi Sh144 kufikia jana.

Kwenye mahojiano na ‘Njenje’, mdadisi wa masuala ya kiuchumi Tony Watima, anasema mwelekeo wa thamani ya shilingi katika miezi michache ijayo utakuwa na athari kubwa kwenye ulipaji madeni na hata kiwango cha maisha nchini.