Kimataifa

Matumaini duniani chanjo ya corona ikipatikana

November 10th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA na CHARLES WASONGA

ULIMWENGU umepata matumaini ya kudhibitiwa kwa janga la Covid-19 baada ya mojawapo ya dawa zilizovumbuliwa kubainika kuwa bora zaidi.

Mnamo Jumatatu, Novemba 9, 2020 kampuni za kutengeneza dawa nza Pfizer na BioNTech zilisema chanjo hiyo mpya imeinika kuwa na asilimia 90 ya uwezo wa kutibu.

Hii ina manaa kuwa tisa kati ya wagonjwa 10 wa Covid-19 waliotumia chanjo hiyo walipata afueni.

Kampuni hizo pia zilisema kuwa dawa hiyo haikuonyesha madhara yoyote kwa wagonjwa waliotumiwa kuifanyia majaribio.

“Leo (Jumatatu) ni siku kubwa kwa sayansi na walimwengu. Matokeo kutoka kwa majiribio matatu yaliyofanyiwa chanjo dhidi ya Covid -19 yameonyesha kuwa inaweza kudhibiti na kuzuia ugonjwa huo,” akasema Dkt Albert Bourla, ambaye ni mwenyekiti na afisa mkuu mtendaji wa kampuni ya Pfizer.

Akaongeza, “Tumepiga hatua hii muhimu katika utengenezaji wa chanjo wakati ambapo ulimwengu unaihitaji zaidi. Hii ni kutokana na sababu kwamba mataifa mengi yameshuhudia ongezeko la visa vya maambukizi na vifo. Hospitali zimejaa wagonjwa wa corona na chumi zilizoathirika ndizo zinajaribu kujiinua tena.”

Pfizer inatarajiwa kuanza kuwapa watu chanjo hiyo nchini Amerika, hawa wale ambao wana umri wa kati ya miaka 16 na 85. Taifa hilo ni mojawapo ya zile ambazo zimeathiriwa zaidi na janga hilo kwa kuandikisha zaidi ya maambukizi 10 milioni na zaidi ya vifo 238,000

Ikiwa chanjo hiyo itasajili hivi karibuni, wahudumu wa afya watakuwa wa kwanza kupewa mwishoni mwa mwaka huu.

Kufikia sasa zaidi ya watu 50 milioni kote ulimwenguni ameambukizwa virusi vya corona huku 1.3 wakifariki. Na wengine 33 milioni wamepona.

Nchini Kenya, zaidi ya wagonjwa 1,000 wamefariki kutokana na Covid-19; wa hivi punde akiwa diwani wa Hell’s Gate, Naivasha John Njuguna maarufu kama Wa Sussy. Na zaidi ya watu 60,000 wameambukizwa virusi vya corona tangu kisa cha kwanza kiliporipotiwa nchini mnamo Machi 13, 2020.