Habari

Matumaini juu idadi ya wanaopona corona ikiongezeka

August 10th, 2020 2 min read

CHARLES WASONGA na SAMMY WAWERU

KWA mara nyingine Kenya imeonekana kupiga hatua nzuri katika vita dhidi ya Covid-19 baada ya kuandikisha idadi ya juu ya waliopona ikilinganishwa na walioambukizwa.

Kulingana na takwimu zilizotolewa na Waziri wa Afya Mutahi Kagwe  akiwa Kericho mnamo Jumatatu, wagonjwa 534 wamepona kwa siku moja huku idadi ya wagonjwa wapya katika muda huo ikiwa 492.

Kupona kwa wagonjwa hao sasa kumefikisha idadi jumla ya waliopona kuwa 13,495 huku idadi jumla ya maambukizi ikiwa 26,926.

Wagonjwa 492 wapya walipatikana baada ya sampuli 4, 603 kufanyiwa uchunguzi. 478 miongoni mwao ni Wakenya huku 14 wakiwa raia wa kigeni,

Miongoni mwa waliopona, 478 walikuwa wakiuguzwa chini ya mpango wa kuwahudumiwa wagonjwa wa corona nyumbani ilhali 56 walikuwa wakipokea matibabu katika hospitali mbalimbali humu nchini.

Hata hivyo, wagonjwa watatu walifariki na hivyo kufikisha 423 idadi ya wagonjwa walioangamizwa na Covid-19

Waziri Kagwe alielezea hofu kwamba idadi ya watoto wanaoambukizwa virusi vya corona inazidi kuongezeka, kwani Jumatatu mtoto mwenye umri wa miezi 11 ni miongoni mwa watu 492 waliothibitishwa kuwa na virusi hivyo.

Kina mama wenye watoto wachanga wametakiwa kudhibiti idadi ya watu wanaowatemebelea.

Mtoto mwenye umri wa miezi 11 ni kati ya waliothibitishwa kuambukizwa virusi vya corona.

Waziri ametangaza kwamba mgonjwa wa umri mkubwa amekuwa na miaka 83.

Aidha, Bw Kagwe ameeleza wasiwasi kuhusu ongezeko la maambukizi ya corona miongoni mwa watoto wenye umri wa chini.

“Taifa linaendelea kuandikisha maambukizi ya corona miongoni mwa watoto hivyo ninahimiza kina mama wanaonyesha na wenye watoto wadogo, mdhibiti kiwango cha watatu wanaowatembelea,” waziri ameshauri.

Bw Kagwe ameonya kuwa ziara za wageni kusalimu watoto waliozaliwa ndizo zinachangia maambukizi.

“Tunaelewa upatapo mtoto wageni huja, lakini tumesema kwa wakati huu wenye hamu ya kusalimia mtoto tunawauliza mtume zawadi kwa njia ya M-Pesa ambayo haitaleta virusi; na baadaye utaenda kumuona,” waziri akasema.

Bw Kagwe amesema visa vya watoto wenye umri mdogo kuendelea kuandikishwa, ni jambo linalotia wizara hofu.

“Haya ni masuala muhimu kwetu, hatutaki watoto kuugua. Kwa hivyo, nawahimiza akina mama wenye watoto waachanga kukoma kuwaalika wageni wengi nyumbani,” akasisitiza.

Kulingana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Afya Nchini, Dkt Patrick Amoth, kufikia sasa Kenya imepoteza mtoto mmoja pekee aliyeangamia akiwa na umri wa miezi sita kutokana na Covid-19.

“Watoto waliozaliwa na wanaoendelea kukua wanafanya vyema,” Dkt Amoth amesema.

Afisa huyo amehimiza watu kula vyakula vyenye madini faafu na kamilifu ili kuimarisha kinga ya mwili, dhidi ya virusi vya corona.

“Hakikisha unakunywa maji mengi, aghalabu zaidi ya lita mbili kwa siku,” Dkt Amoth akashauri. Alisisitiza haja ya watu kuota miale ya jua, hasa majira ya asubuhi ili kuimarisha mifupa.

Watu pia wamehimizwa kupata lepe la usingizi wa kutosha, Dkt Amoth akipendekeza zaidi ya saa nane kwa siku.

Katika visa 492 vya Jumatatu, 478 ni Wakenya huku 14 wakiwa raia wa kigeni. Idadi hiyo imefikisha jumla ya visa 26, 928 vya maambukizi ya Covid-19 nchini.

Jumla ya sampuli 358,330 ndizo zimefanyiwa vipimo kufikia sasa. Jumatatu, chini ya saa 24 zilizopita wagonjwa 534 walithibitishwa kupona corona, huku watatu wakiripotiwa.