Matumaini kiungo Jack Grealish wa Aston Villa atacheza dhidi ya Leeds United katika EPL

Matumaini kiungo Jack Grealish wa Aston Villa atacheza dhidi ya Leeds United katika EPL

Na MASHIRIKA

MKUFUNZI Marcelo Bielsa wa Leeds United amesema anatarajia nahodha Jack Grealish atakuwa sehemu ya kikosi kitakachotegemewa na Aston Villa dhidi yao katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) itakayochezewa uwanjani Elland Road.

Grealish hakuwa sehemu ya timu ya Villa iliyopokezwa kichapo cha 2-1 kutoka kwa Leicester wikendi iliyopita baada ya sogora huyo raia wa Uingereza kupata jeraha la mguu lililotarajiwa kumweka nje ya kikosi cha kocha Dean Smith kwa muda mrefu.

“Grealish, 25, ni mchezaji wa haiba kubwa aliye na uwezo wa kuvuruga mpango wa kila mpinzani wa Villa. Hata hivyo, kuwapo kwake kambini mwa Villa kunaweza kuwapa wapinzani motisha zaidi na kuondoka uwanjani na alama muhimu,” akasema kocha Bielsa ambaye ni raia wa Argentina.

“Kucheza dhidi ya wapinzani wanaojivunia wachezaji wao wote wa kikosi cha kwanza ni jambo zuri kwa kuwa litatupa ari ya kujituma zaidi. Kuingia ugani ukifahamu kwamba wapinzani hawatakuwa na baadhi ya wanasoka wao tegemeo hushusha kiwango cha motisha ya kikosi kinachocheza nao, nasi Leeds United tusingependa iwe hivyo,” akaongeza Bielsa.

Kufikia sasa, Leeds United wanashikilia nafasi ya 10 kwa alama 35 baada ya mechi 25 za ufunguzi wa msimu. Waliwapepeta Southampton 3-0 katika mechi yao ya awali. Ni pengo la pointi moja pekee ndilo linawatenganisha na nambari nane Villa waliopokezwa kichapo cha 3-0 kutoka kwa Leeds United mnamo Oktoba 2020.

Ingawa hivyo, nafuu zaidi kwa Villa ya kocha Smith ni kwamba wana mechi mbili zaidi za kusakata ili kufikia idadi ya michuano ambayo imepigwa na Leeds.

Pigo zaidi kwa mkufunzi Bielsa atakayemkaribisha kiungo Mateusz Klich, ni kwamba atakuwa bila huduma za wanasoka Kalvin Phillips, Rodrigo na Robin Koch katika kikosi kitakachovaana na Villa.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Timu ya Kenya ya marathon ya Olimpiki yapigwa jeki na Sh1m...

Kiambu yaendelea kujiimarisha katika ufugaji wa samaki