Matumaini tele kiwanda cha sukari kianze kunguruma tena

Matumaini tele kiwanda cha sukari kianze kunguruma tena

Na SHABAN MAKOKHA

KIWANDA cha sukari cha Mumias ambacho hakijakuwa kikihudumu kwa muda wa miaka mitatu baada ya kuporomoka, huenda kikaanza kusaga sukari hivi karibuni kwa kuwa mchakato wa kukikodisha kwa mwekezaji unakaribia kuanza.

Tangu Septemba, 2019, kiwanda hicho kimekuwa chini ya urasimu wa benki ya KCB ambayo ilijukumika zaidi kulinda rasilimali zake na kufufua operesheni zake.

Meneja wa KCB P.V. Ramana Rao alianzisha mchakato wa kukodisha kiwanda hicho ila shughuli hiyo ikaingiliwa na wanasiasa wakiongozwa na Seneta wa Kakamega Cleophas Malala aliyedai kuwa mchakato wa kumpata mwekezaji mpya haukuwa na uwazi.

Kutokana na malalamishi ya Bw Malala, Kamati ya Seneti kuhusu Kilimo iliamuru kuwa mchakato huo uanze upya tena kwa njia ya uwazi.

Isitoshe kulikuwa na kesi mahakamani iliyowasilishwa na Chama cha Ushirika cha Gakwamba ambacho kilitaka meneja huyo wa KCB asikubaliwe kuchapisha matangazo ya tenda.

Katibu wa Muungano wa Wafanyakazi na Wakulima wa Miwa (KUSPAW) Francis Wangara alisema kuwa wanasubiri mwelekeo kutoka kwa Bw Rao kufahamu hatua inayofuata baada ya muda wa kupokea tenda na kuzitathmini kukamilika.

“Baada ya tenda kufunguliwa wiki jana, tuna imani kuwa hakutakuwa na utata zaidi kuhusu kufufua kiwanda cha Mumias,” akasema Bw Wangara.

You can share this post!

Unywaji pombe unachangia matatizo ya akili – Nacada

Kenya yapokonya wavuvi wa China leseni kwa kutesa Wakenya