Habari Mseto

Matumaini visa vya corona nchini vikipungua

August 30th, 2020 1 min read

Na WANDERI KAMAU

IDADI ya visa vya maambukizi ya virusi vya corona inaendelea kupungua nchini, hali inayoibua matumaini kwamba huenda hali ya kawaida ikarejea miongoni mwa Wakenya hivi karibuni.

Jumamosi, watu 164 walithibitishwa kuambukizwa virusi, idadi ambayo ni ya chini ikilinganishwa na hali ilivyokuwa majuma kadhaa yaliyopita.

Inafikisha idadi ya jumla ya watu walioambukizwa kuwa 33,794.

Watu 156 walithibitishwa kupona, na kufikisha dadi ya waliopona nchini kuwa 19,590.

Hata hivyo, watu watano zaidi waliaga dunia, jumla ya wale waliofariki ikifikia 572.

Kwenye hotuba yake kwa nchi Jumatano, Rais Uhuru Kenyatta, alieleza kuridhishwa na mwelekeo huo, akisema ni ishara kwamba huenda visa hivyo vikapungua maradufu.

Hata hivyo, Waziri wa Afya, Mutahi Kagwe, alisema mwelekeo kamili kuhusu virusi hivyo utaamuliwa na hali itakavyokuwa nchini kwa majuma mawili yajayo.