Michezo

Matumaini ya Atletico kucheza UEFA yafifia

June 14th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

ATLETICO Madrid waliridhika na alama moja baada ya kulazimishiwa sare ya 1-1 na Atletico Madrid katika mechi ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) uwanjani San Mames mnamo Jumapili.

Kivumbi hicho kilikuwa cha kwanza cha vikosi hivyo kushiriki baada ya likizo ya miezi mitatu iliyosababishwa na janga la corona.

Matokeo hayo yalididimiza zaidi matumaini ya Atletico kufuzu kwa kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao.

Chini ya kocha Diego Simeone, Atletico kwa sasa wanashikilia nafasi ya sita jedwalini kwa alama 46 sawa na Getafe waliopokezwa kichapo cha 2-1 na Granada mnamo Juni 12.

Iker Muniain aliwaweka Bilbao kifua mbele kunako dakika ya 37 kabla ya Atletico kusawazisha mambo dakika mbili baadaye kupitia kwa Diego Costa aliyekamilisha kwa ustadi krosi ya Jorge Koke.

Atletico nusura wapachike wavuni bao la ushindi mwanzoni mwa kipindi cha pili baada ya kipa Unai Simon kulitema kombora la Renan Lodi na kurejesha mpira kwa Santiago Arias aliyepoteza nafasi ya wazi.

Ni pengo la alama nne ndilo linalowatenganisha Atletico na Sevilla waliopaa hadi nafasi ya tatu mnamo Juni 11 baada ya kuwapepeta Real Betis 2-0 kwenye gozi la uwanjani Ramon Sanchez-Pizjuan.

Barcelona waliowachabanga Mallorca 4-0 wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 61, mbili zaidi kuliko watani wao wa tangu jadi Real Madrid waliosalia katika nafasi ya pili baada ya kuwacharaza Eibar 3-1.