Michezo

Matumaini ya Kawangware Utd kuhifadhi ubingwa yazimwa

September 24th, 2018 1 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

Matumaini ya Kawangware United kuhifadhi ubingwa wa taji la Super 8 Premier League yaliyeuka mwishoni mwa wiki baada ya kutoka sare 1-1 na Team Umeme.

Nafasi ya kuwania taji hilo sasa imebakia mikononi mwa timu tatu- Jericho All Stars, Makadara Junior League SA na Technical University of Kenya (TUK).

Kawangware walihitaji ushindi katika mechi hiyo na kuomba dua, Jericho washindwe na Shauri Moyo Blue Stars ili kuhifadhi matumaini yao, lakini ushindi wa Jericho wa 8-0 dhidi ya Blue Stars uwanjani Camp ulivuruga matumaini yao.

Joseph Makori aliifungia Umeme mapema katika mechi hiyo kabla ya Wellington Hodari kusawazishia watetezi dakika ya 35.

Kawa sasa mabingwa hao wanakamata n afasi ya tano, tofauti ya pointi 17 nyuma ya Jericho walio na pointi 58 huku zikibakia mechi nne. Hata hivyo, vijana hao kutoka Dagoretti wangali na matumaini ya kumaliza mingoni mwa tatu bora.

“Hatukuweza kuvuma kama ilivyotarajiwa kwa sababu tumesajili wachezaji kadhaa wapya kwa ajili ya kujenga kikosi cha baadaye,” alisema naibu wa kocha wa kikosi hicho, Laban Mwangi.

Jospeh Makori wa Umeme (kushoto) akiwania mpira dhidi ya Michael Kiarie wa Kawangware United. Picha/ John Ashihundu

Kwa upande mwingine, Vincent Paul wa Jericho alisema: “Tulipata nafasi nyingi lakini hatufanikiwa kufunga mabao. Tunahitaji kuimarika na kutumia nafasi zote katika mechi za usoni.”

Kelvin Ndungu wa Jericho All Stars anayeongoza kwa ufungaji mabao aliongeza idadi yake kufikia mabao 20 baada ya kufanikiwa kubachika wavuni mabao manne mwsihoni mwa wiki, huku mpinzani wake mkuu Bundu Engo akifunga matatu.

Uwanjani Kabete, TUK walilazimika kutoka sare 0-0 na Shauri Moyo Sporttif ambao kwa sasa wanakamata nafasi ya nane wakiwa na pointi 34.

Matokeo ya mechi kwa ufupi: Kayole Asubuhi 0 Metro Sports 0; Makadara Junior League SA 4 Meltah Kabiria 1; Zamalek 2 Leads United 0; Team Umeme 1 Kawangware United 1; Rongai All Stars 1 RYSA 0; TUK 0 Shauri Moyo Sportiff 0; Jericho All Stars 8 Shauri Moyo Blue Stars 0.