Michezo

Matumaini ya mdhamini Ligi Kuu yayeyuka

January 10th, 2020 2 min read

Na CECIL ODONGO

KLABU za Ligi Kuu nchini (KPL) zimetakiwa zijitayarishe kwa nyakati ngumu zaidi kwa sababu hakuna matumaini ya mdhamini mpya kupatikana hadi ligi hiyo ikamilike msimu huu.

Mwenyekiti wa KPL Ambrose Rachier alieleza ‘Taifa Leo’ juma hili kwamba hakuna matumaini ya kupata mdhamini mpya na wale walioonyesha nia, walikuwa wakitoa pesa kidogo ambazo hazitoshi kuendesha ligi na kufadhili timu zote 18.

Kwa mujibu wa Rachier ambaye pia ni mwenyekiti wa Gor Mahia, walishindwa kuafikiana na kampuni hizo zilizotoa hela chache, kwa sababu zilidai mechi za KPL hazipeperushwi katika vyombo vya habari vya kimataifa.

Hata hivyo, hakufafanua iwapo KPL inafaa kusimamishwa kwa sababu taji la msimu huu bado halijanunuliwa na pia itakuwa vigumu kumtuza mshindi kwa sababu ya ukosefu wa mdhamini.

Masaibu ya KPL yanatokota zaidi ikizingatiwa kwamba washindi wa taji la msimu uliopita Gor Mahia bado hawajapokezwa kitita chao hadi leo.

“Ligi ya KPL iko mashakani na hali ya sasa huenda isibadilike. Hakuna dalili zozote kwamba ligi itapata mdhamini msimu huu. Waliotaka kuidhamini walikuwa wakitoa pesa kidogo ambazo hazitoshi klabu zote 18.

“Vilevile walilalama kwamba hawangepata faida sana kwa sababu mechi zetu hazipeperushwi kwenye runinga mbalimbali za kimataifa kama za nchi nyingine. Ni hali ya kusikitisha lakini hatuna budi ila kuikubali,” akasema Rachier.

Alithibitisha kwamba KPL ililazimika kuhamisha afisi zake kutoka Westlands hadi barabara ya Lenana ili kupunguza gharama ya matumizi kwa sababu haingeweza kumudu kodi inayotozwa.

Kauli ya Rachier inajiri baada ya timu tatu za KPL kukosa kufika uwanjani katika mechi sita huku Nzoia Sugar FC ikiwa timu ya hivi punde kukosa mechi yao dhidi ya Bandari, mjini Mombasa wikendi iliyopita.

SoNy Sugar ambayo ilikosa mechi zake tatu dhidi ya Zoo Kericho, Tusker na AFC Leopards tayari imeondolewa ligini huku Chemeli iliyosajili ushindi wake wa kwanza msimu huu kwa kuchapa Nzoia 1-0 ikikosa mechi dhidi ya Bandari na KCB.

Hali imekuwa ngumu kifedha kwa KPL baada ya Sportpesa kuondoa ufadhili wake Agosti 2019 kisha kusitisha biashara zake nchini baada ya kukosa kuelewana na serikali kuhusu ushuru kampuni hiyo ya kamari ilifaa kutozwa.