Matumaini ya mwafaka kati ya Israeli na Palestina yafifia

Matumaini ya mwafaka kati ya Israeli na Palestina yafifia

Na MASHIRIKA

JERUSALEM, Israeli

JUHUDI za kutafuta mwafaka wa amani kati ya Israeli na Wapalestina zimegonga mwamba, licha ya viongozi katika sehemu mbalimbali duniani kuzirai pande hizo mbili kusitisha vita hivyo.

Kulikuwa na matumaini Jumanne kuwa pande hizo zingesitisha mashambulio, hasa baada ya Amerika kusema inaunga mkono mwafaka wa amani.

Hata hivyo, duru katika jeshi la Israeli zilisema hakuna “ajenda yoyote ya kusitisha mapigano hayo waliyowasilishiwa.”

Baadhi ya nchi kama Ufaransa, Misri na Jordan zimeliomba Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) kuchukua hatua za haraka kuhakikisha mapigano hayo yamesitishwa.

“Kuna juhudi za kichinichini zinazoendelea kuona ikiwa kuna mwafaka utakaofikiwa na kutangazwa hadharani wakati ufaao utakapowadia,” akasema Katibu wa Ikulu ya White House, Jen Psaki.

Wakati huo huo, viongozi wakuu wa kundi la Hamas nchini Qatar walisema kuwa “juhudi za kutafuta mwafaka wa kusitisha mapigano zinaendelea.”

Hata hivyo, waliilaumu Israeli kwa kuwa “sumbufu” kwa kutoa sharti kuwa lazima kundi hilo lisitishe mashambulio hayo kwanza ili itathmini ikiwa itachukua hatua kama hiyo.

Mark Regev, aliye mshauri wa Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu, alisema taifa hilo “linataka pawepo na mwafaka utakaoleta suluhisho la kudumu.”

Hilo linajiri huku ndege za kivita za Israeli zikiendelea kufanya mashambulio katika ukanda wa Gaza, Jumatano.

Kwenye mashambulio ya Jumatano, Wapalestina wanne waliuawa, miongoni mwao akiwemo mwanahabari.

Hakukuwa na ripoti zozote kuhusu majeruhi.

Kwenye shambulio jingine la awali, wanajeshi wa Israeli waliwaua Wapalestina wanne kwa kuwapiga risasi. Walikuwa wakishiriki kwenye maandamano katika maeneo ya West Bank na Mashariki mwa Jerusalem.

Hilo lilifikisha idadi ya Wapalestina waliouawa tangu mashambulio hayo kuanza kufikia 219. Miongoni mwa waliouawa ni watoto 63. Wapalestina zaidi ya 1,500 wamejeruhiwa.

Waisraeli 12 wameuawa, miongoni mwao wakiwemo watoto wawili. Waisraeli 300 wamepata majeraha.

Jumatano, mamia ya familia za Wapalestina zilianza harakati za kuwaokoa jamaa na bidhaa zao kutoka Jumba la Al-Andalus, jijini Gaza, baada kupata ripoti za kijasusi kwamba jumba hilo lingeshambuliwa na ndege za kivita za Israeli.

Hofu ilizuka baada ya moshi kuonekana ukitoka kwenye jengo hilo.

Kufikia sasa, zaidi ya shule 50 katika eneo la Gaza zimeharibiwa kutokana na msururu wa mashambulio yanayoendelezwa na ndege za Israeli, kulingana na shirika la kuwatetea watoto la Save the Children. Hali hiyo imewaathiri zaidi ya watoto 41,000.

Nchini Israeli, ni shule tatu pekee zilizoharibiwa kufuatia roketi zinazorushwa na makundi ya kigaidi kama Hamas.

You can share this post!

Watabiri hewa Pwani wachanganya wakazi

TAHARIRI: Koome aonyeshe hapokei maagizo