Bambika

Matumaini ya Pasta Kanyari kumuoa tena Betty Bayo yauma mchanga

June 14th, 2024 1 min read

NA FRIDAH OKACHI

MWANAMUZIKI wa Injili Beatrice Mbugua almaarufu Betty Bayo amewashauri wanaotafuta wapenzi wa kudumu, kumuenzi Mungu na kupata mke aliye na sifa za kuomba.

Hii ni baada ya aliyekuwa mumewe wa zamani Victor Kanyari Kimani (Pasta Kanyari) kujitokeza na kueleza kuwa ana imani kuwa Betty Bayo angerejea kwake.

Katika Mahojiano na Taifa Leo, Betty Bayo alionyesha kuridhika na uhusiano alio nao kwa sasa.

“Nipo sawa mahali nilipo. Kwa wale wanaomwamini Mungu na kutamani ndoa ya kudumu, Mungu ndiye hupatiana. Na Mungu awape wapenzi wa maombi wala sio kitu cha maombi,” alisema Betty Bayo.

“Miaka miwili iliyopita niliondoka kwenye soko baada ya mimi na mchumba wangu kufanya sherehe ya kitamaduni (Ruracio),” aliongeza Betty Bayo.

Mama huyo wa watoto watatu, ambaye amekuwa kwenye mahusiano hayo mapya kwa miaka minne sasa alisema kuwa kupakia picha hiyo ni baada ya mpenziwe kumpa idhini.

“Mwanzo tukianza mahusiano hakuwa sawa kumpakia kila mahali au kuzungumza kumhusu. Lakini wakati umefikia mmfahamu kidogo tu,” alisema Betty.

Hivi majuzi Betty Bayo aliingia kwenye mitandao ya kijamii na kupakia picha akiwa na mpenziwe almaarufu Tash na mwanawe. Msanii huyo, alipata uungwaji mkono kutoka kwa wafuasi wake, ambao wengi wao walimtaka asifikirie kurudiana na Kanyari.

Wafuasi wake pia walieleza kuwa msanii huyo, alionekana kuwa na furaha zaidi na mpenzi wa sasa ambaye ameendelea kumtia moyo na kuendelea kusonga mbele katika uhusiano wao.

Picha hiyo ilipakiwa muda tu baada ya Pasta Kanyari kushiriki kwenye mahojiano akiwa na wingi wa matumaini ya kuungana tena na aliyekuwa mkewe.

Kwenye mahojiano hayo, pasta huyo alishikilia kuwa tangu kuachana, Betty Bayo hajawahi kupata mtoto na mwanamume mwingine tangu talaka yao ilipotangazwa.

“Nina imani atakuja rejea kwangu. Nina uhakika tangu kuachana kwetu hajawahi fanikiwa kupata mtoto na mwanamume mwingine,” alisema Pasta Kanyari.