Habari

Matumaini ya Sonko kujiokoa yamo kortini tu

November 30th, 2020 2 min read

Na COLLINS OMULO

GAVANA wa Nairobi, Mike Sonko kwa mara nyingine ameelekea kortini ili kujinnusuru huku hoja ya kumtimua ikitarajiwa kuwasilishwa Alhamisi katika Bunge la Kaunti.

Huku akikimbilia kortini kusalia uongozini, madiwani nao wameapa kumtimia kwa kuunga mkono hoja hiyo inayodhaminiwa na Kiongozi wa wachache Michael Ogada.

Kinaya ni kwamba mnamo Ijumaa, Bw Sonko alionekana kulegeza msimamo huku akikumbatia mbinu mbalimbali za kujiokoa ikiwemo kuwafikia Rais Uhuru Kenyatta na Kinara wa ODM Raila Odinga.

Hata hivyo, Bw Sonko sasa anashikilia kuwa yupo tayari kuendelea na maisha yake hata bila kuwa gavana, lakini hatatia saini bajeti ya kaunti ili kulipokeza Shirika la Huduma kwa wakazi wa jiji (NMS) Sh27.5 bilioni.

“Sihitaji kuokolewa. Nitaendelea kusimama wima kama seneti wakati ambapo ilichukua msimamo kuhusu mswada wa ugavi wa mapato. Sitatia saini na kupokeza fedha kwa shirika ambalo halina msingi wa kisheria,” akasema Bw Sonko.

Kupitia wakili wake Harrison Kinyanjui, Gavana Sonko anamshutumu Spika Benson Mutura kwa kukaidi agizo la korti na kukubali hoja nyingine ya kumtimua iwasilishwe ilhali uhalali wa ile ya awali iliyowasilishwa Februari, bado haujaamuliwa na mahakama.

“Kesi ya kupinga kuwasilishwa kwa hoja ya awali bado ipo mahakamani na uamuzi wake bado haujatolewa. Kesi hiyo itasikizwa kortini Disemba 3, 2020 na bado inaendelea,” akasema Bw Kinyanjui kwenye barua kwa Bw Mutura Novemba 27, 2020.

Hata hivyo, Bw Mutura anasema hoja hiyo ya Februari iliyowasilishwa na diwani wa Makongeni Peter Imwatoka iliondolewa kwa kukosa kufuata kanuni za bunge la kaunti.

“Kwa kuwa Imwatoka alikosa kukamilisha uwasilishaji wa hoja hiyo kwa wakati unaotakikana kisheria, naamuru hoja yake imeondolewa kulingana na kanuni za bunge hili,” akasema Bw Mutura.

Hata hivyo, Bw Kinyanjui anadai ni Bw Imwatok pekee ambaye anaweza kuondoa hoja hiyo kwa kuwa sheria za bunge la kaunti zinaamrisha hivyo.

“Kanuni za bunge zinaamrisha kuwa hoja spesheli ya kumwondoa gavana afisini inaweza kuondolewa tu na mwasilishaji. Kwa hivyo, spika hana mamlaka ya kuondoa hoja hiyo iwapo haikuondolewa na Bw Imwatok Februari,” akasisitiza wakili huyo.