Michezo

Matumizi ya pufya yalivyotisha kusambaratisha sifa ya Kenya

January 1st, 2020 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

KERO la matumizi ya dawa za kusisimua misuli katika michezo ya Kenya lilizidi kuandama wanamichezo wake, hasa wanariadha mwaka 2019.

Takwimu za mwaka huu kutoka kwa Kitengo cha Maadili cha Riadha katika Shirikisho la Riadha Duniani (AIU), zinazonyesha Kenya ikiwa miongoni mwa mataifa yanayohangaishwa sana na udanganyifu huo michezoni.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Kukabiliana na Matumizi ya Pufya Duniani (WADA), wanariadha 15 kutoka Kenya walipatikana na hatia ya kutumia dawa hizo haramu mwaka 2019.

Wote wanatumikia marufuku ya kati ya miaka miwili na minane, kwa sababu ya kujaribu kutumia udanganyifu kupata ufanisi.

Imefichuka kuwa Wakenya wanapenda sana kutumia dawa aina ya EPO ambayo husababisha kuongezeka kwa seli nyekundu za damu zinazosafirisha oksijeni ndani ya mwili, na hivyo kumpa mkimbiaji uwezo wa kupumua vyema zaidi.

Dawa zingine zinazotumiwa na Wakenya kwa wingi ni norandrosterone, prednisone, salbutamol na homoni za kuongeza maumbo ya mwili (steroid).

Mataifa ya India, Morocco, Uchina, Marekani, majirani wa Kenya, Ethiopia, na Afrika Kusini pia wako katika orodha ya nchi ambazo wanamichezo wake wamenaswa katika udanganyifu huo.

Mapema Desemba 2019, WADA ilipiga Urusi marufuku kushiriki mashindano yoyote kwa kipindi cha miaka minne, kutokana na zogo la uovu huo kukita mizizi nchini mwake.

Orodha ya Wakenya waliopigwa marufuku mwaka 2019 inajumuisha malkia wa Jumuiya ya Madola katika mita 10,000 Joyce Chepkirui; mshikilizi wa zamani wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 21 Abraham Kiptum; mshindi wa zamani wa Jumuiya ya Madola mbio za mita 10,000 Lucy Kabuu; malkia wa Tokyo Marathon mwaka 2017 Sarah Chepchirchir; na mfalme mara tatu wa mbio za mita 1,500 Asbel Kiprop.

Wengine ni Jacob Kendagor, Salome Biwott, Cyrus Rutto, Felix Kirwa, Hilary Yego, Samson Mungai Kagia na Vincent Yator.

Marufuku ya bingwa wa Olimpiki Jemimah Sumgong, ambaye alikuwa ameadhibiwa mwaka 2017, pia iliongezwa Januari 2019 hadi miaka minane.

Ripoti ya WADA iliyotolewa Septemba 2018 inasema kuwa, kutoka mwaka 2004 hadi Agosti 2018 wanariadha 138 wa Kenya walifeli vipimo vya matumizi ya dawa za kusisimua misuli.

Cha kushangaza ni kuwa visa vya matumizi ya dawa hizo haramu viliongezeka 2019, mwaka mmoja baada ya Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) kuzidisha vita dhidi ya uovu huo.

AK ilianzisha warsha ya kuleta pamoja wanariadha ili kuwapa hamasisho kuhusu dawa hizo pamoja na mbinu za kuepuka mitego ya maajenti walaghai wanaotaka kuwatumbukiza katika pufya.

Warsha hizo zitakakuwa zikifanyika kila mwisho wa mwaka. Makala ya kwanza yaliandaliwa mwaka 2018 mjini Nairobi na kuhudhuriwa na wanariadha 150.

Idadi ya wanariadha waliohudhuria makala ya pili mwaka 2019, yaliyoandaliwa Desemba 6 mjini Eldoret, iliongezeka mwaka 2019 hadi kuwa 300.

Malengo mengine ya mkutano huo ni kuelimisha wanariadha kuhusu jinsi ya kuwekeza mapato yao, kando na kuwarai kushiriki mashindano bila ya kutumia njia za mkato kupata mafanikio.

Kenya, ambayo tangu mwaka 2016 imekuwa katika orodha ya mataifa yanayovunja sana sheria zinazokataza matumizi ya pufya michezoni, inaandaa mikakati ya kuweka sheria itakayowafunga pia makocha na maajenti wa watimkaji wakosaji, ifikapo katikati ya mwaka 2020.

Uovu huo umefanya mashabiki wengi wa riadha nchini Kenya kusherehekea ushindi wa wanariadha wao shingo upande kwa sababu hawana uhakika wanachosherehekea ni halali ama la.