Matusi dhidi ya Raila yamwandama Uhuru

Matusi dhidi ya Raila yamwandama Uhuru

Na LEONARD ONYANGO

MATAMSHI ya zamani ya Rais Uhuru Kenyatta ya kumdhalilisha Kiongozi wa ODM Raila Odinga yamegeuka kuwa kizingiti kikubwa katika juhudi zake za kumpigia debe kuwa mrithi wake 2022.

Wakati wa kampeni za 2017, Rais Kenyatta alimtaja Bw Odinga kama kibaraka wa mataifa ya Magharibi, asiyependa maendeleo, mpenda vurugu, mzee na ‘mwendawazimu’ asiyefaa kupewa nafasi ya uongozi. Lakini sasa Rais Kenyatta anasisitiza kuwa Bw Odinga ndiye ataweza kuendeleza miradi ya maendeleo baada yake kustaafu mwaka ujao.

Hii ni kinyume na awali ambapo alimshinikiza Bw Odinga kustaafu siasa akisema kuwa alikuwa mzee sana. Rais Kenyatta pia alidai kuwa Bw Odinga ndiye alitatiza maendeleo katika serikali ya mseto iliyobuniwa baada ya ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.

“Kati ya 2002 na 2007, Mzee Kibaki alifanikiwa kukuza uchumi kwa asilimia nane. Lakini huyu mtu (Raila) alipoleta vurugu baada ya uchaguzi wa 2007 na kuingia katika serikali, kasi ya ukuaji wa uchumi iliporomoka hadi asilimia 0.5.

“Sasa mimi na ndugu yangu (Ruto) tunapojaribu kuinua uchumi, huyu mtu (Raila) analeta kelele ati fedha zinaibwa, vitendawili na uongo,” alisema Rais Kenyatta.Matamshi hayo sasa yanamtatiza Rais Kenyatta kuyafuta katika akili za wengi wa wafuasi wake.

Wiki iliyopita alivunja kauli yake ya awali kuwa Bw Odinga ni mzee ambaye hafai kuwa rais, aliposema kuwa umri si hoja katika uongozi bali kinachohitajika ni upevu wa akili na tajriba.“Unaweza kuanza kampeni mapema kwa kasi lakini hivi karibuni utaishiwa na nguvu na uliyedhani kuwa ni mzee akupite,” akasema Rais Kenyatta akiwa Nakuru, akimrejelea naibu wake William Ruto.

Kuomba Msamaha

Sasa wandani wa Rais Kenyatta wanajuta kwa matamshi hayo na wamekuwa wakitumia kila fursa yoyote wanayopata kuomba msamaha kwa kuzungumza ‘mambo machafu na ya uongo’ dhidi ya Bw Odinga.“Tulikuwa tunasingizia mzee mambo mengi ya uongo kwa sababu alikuwa akishindana na mmoja wetu…sisi Baba (Raila) tunaomba msamaha.

“Kwa niaba ya watu wa Mlima Kenya, ule uongo wote tulikuwa tumekuwekea kwa miaka mingi tunaomba msamaha. Najua umetusamehe.“Kwa sababu umetusamehe, 2022 tutarudisha mkono kwa sababu ulisimama na Mwai Kibaki 2002 na baba yako alisimama na Mzee Jomo Kenyatta,” akasema Mbunge wa Kieni, Kanini Kega.

Wadadisi wanasema kuwa matamshi hayo ya Rais Kenyatta pamoja na viongozi wengine yamechangia katika ugumu wanaokumbana nao wanapomuuza Bw Odinga katika eneo la Mlima Kenya. Bw Odinga, ambaye anaungwa mkono na mabwanyenye kutoka Mlima Kenya pamoja na Rais Kenyatta, amekuwa akifanya ziara za mara kwa mara katika eneo hilo kwa lengo la kujipatia uungwaji mkono.

Hata hivyo, Rais Kenyatta hayupo peke yake kwenye meli ya vinyonga wa siasa. Baada ya Dkt Ruto na Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru kurushiana cheche za maneno kwa muda mrefu sasa ni marafiki. Uhasama baina ya viongozi wawili hao uliibuka 2016 baada ya Bi Waiguru kumhusisha Dkt Ruto na sakata ya wizi wa Sh1.8 bilioni za Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS).

Mwaja jana maseneta wanaoegemea mrengo wa Dkt Ruto walihimiza kuondolewa mamlakani kwa Bi Waiguru, ambaye alikuwa ametimuliwa na madiwani wa Kaunti ya Kirinyaga kwa madai ya matumizi mabaya ya mamlaka na ufisadi.

Lakini sasa Bi Waiguru ni kati ya magavana wachache nje ya Bonde la Ufa ambao wamejitokeza hadharani kumuunga mkono Dkt Ruto.Dkt Ruto ambaye kabla ya uchaguzi wa 2017 alimtetea vikali waziri wa usalama Dkt Fred Matiang’i baada ya kulaumiwa na upinzani kwa kutumia kisiasa maafisa wa polisi, ndiye sasa anashinikiza waziri huyo atimuliwe kwa madai ya kupanga njama ya kuiba kura 2022.

Khalwale na Ruto

Miezi michache kabla ya uchaguzi wa 2017, aliyekuwa Seneta wa Kakamega Boni Khalwale alimtaka Dkt Ruto kuelezea Wakenya mahali alipata mamilioni ya fedha ambayo alikuwa akigawa makanisani kila wiki. Lakini leo, Bw Khalwale ni miongoni mwa viongozi ambao Dkt Ruto anawategemea kumsaidia kupata kura za urais katika eneo la Magharibi.

Mnamo Aprili 17, 2016, aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnson Muthama alifichua orodha ndefu yenye maovu aliyodai yalitekelezwa na Dkt Ruto.Lakini sasa, Bw Muthama ndiye mwenyekiti wa chama cha United Democratic Alliance (UDA), ambacho Dkt Ruto anatarajiwa kutumia kuwania urais mwaka ujao.Umoja wa Wapwani

You can share this post!

Barrow kutawala kwa muhula wa 2

Magoha asisitiza sharti kiboko kirejee shuleni

T L