Habari Mseto

Matusi ya pasta Ng'ang'a yashtua Wakenya

June 1st, 2019 1 min read

Na BENSON MATHEKA na WANDERI KAMAU

MHUBIRI mbishi James Ng’ang’a wa Kanisa la Neno Evangelism Centre jijini Nairobi, amekasirisha Wakenya tena kwa kuwatusi mapasta wanaohudumu chini yake na kuwalaumu kwa kutomheshimu mkewe.

Kwenye video inayosambazwa mitandaoni, kasisi huyo ambaye anaonekana mwenye hasira, analalamika kwamba baadhi ya maaskofu wamekuwa wakimkosea heshima yeye na mkewe, licha ya kutajirikia katika kanisa lake.

“Mlikuja katika kanisa langu na wake zenu bila chochote. Mmetajirikia hapa, sasa mmeanza kunikosea heshima. Nitawafukuza katika kanisa hili na kufunga makanisa mnayoyaongoza. Hamuwezi kunitisha hata kidogo. Mtanijua mimi ni nani,” anafoka kasisi huyo.

Hivyo, anawataka “kuheshimu agizo lolote analotoa bila kuuliza maswali.”

“Nikisema lolote, mnaitikia na kulikubali bila maswali. Hakuna mshirika wa kanisa hili anayeweza kuniuliza swali. Mimi ndiye mwanzilishi wake,” anasema kwa hasira.

Alitaja makanisa ya mapasta hao kama viosk na kuapa kuwaonyesha cha mtema kuni.

“Wakati huu sasa nitawaonyesha nguvu zangu, mwanamke yeyote akikataa kumheshimu mke wangu… Mlinipata hapa mkiwa na wake wenu, mmetajirika kupitia bidii yangu. Wajinga, vichwa ngumu,” anateta pasta Ng’ang’a.

Mkokoteni

Anaendelea kusimulia kwamba alianza kuhubiri akitumia mkokoteni.

“Ninaapa mbele ya Mungu nitawaonyesha Ng’ang’a ni nani.”

“Nikikohoa, ni lazima mjibu,” anafoka na kudai kwamba shetani anataka kuporomosha kanisa lake.

“Shetani ananipiga vita kwa sababu anataka kuniporomosha, hamuwezi kunitisha… Mimi ndiye Neno na ndio sababu ninapigwa vita… Sitakubali nyinyi na wake wenu mnisumbue,” anaendelea.

Anawaonya kuwa atawafukuza na kufunga makanisa yao yote abaki na la Nairobi.

“Nitawafukuza nyinyi wote takataka,” anaendelea na kuwataja kama watu duni wasio na heshima.

Hii si mara ya kwanza kwa kasisi huyo kuzua vituko na kuacha Wakenya na maswali.

Mnamo Machi, Pasta Ng’ang’a alikamatwa na polisi kwa kumtisha mwanahabari Linus Kaikai wa runinga ya Citizen kufuata maoni yake akipendekeza viongozi wa makanisa kupigwa msasa.