Habari

Mau itammeza Ruto?

August 31st, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

MPANGO wa serikali wa kuwafurusha watu kati ya 40,000 na 60,000 kutoka kwenye vipande vya ardhi vilivyo ndani ya msitu wa Mau, sasa ni jinamizi kwa Naibu Rais William Ruto katika azma yake ya kuingia Ikulu 2022.

Ufurushaji huo huenda ukamweka pabaya Dkt Ruto machoni pa wakazi ambao wanasubiri kuona ikiwa ataunga mkono hatua ya serikali anayotumikia au atawatetea kwa kuwa eneo hilo ni ngome yake ya kisiasa.

Maeneo ambako shughuli hiyo itaendeshwa ni wadi za Ololulunga, Melelo, Sogoo na Segemian ambazo ziko katika kaunti ndogo ya Narok Kusini, kaunti ya Narok.

Jumla ya shule 15 za umma zitabomolewa na tayari Kamishna wa Ukanda wa Rift Valley George Natembeya amesema shule hizo hazifai kufunguliwa Jumatatu kwa muhula wa tatu.

Japo kufikia sasa Dkt Ruto mwenyewe hajalizungumzia suala hilo, kundi la viongozi kutoka Rift Valley wakiongozwa na kiongozi wa wengi katika Bunge la Seneti Kipchumba Murkomen wamepinga ufurushwaji huo wakisema eneo lengwa sio sehemu ya msitu wa Mau.

“Hii ni sehemu ambako kuna zaidi ya wadi tatu na shule kadha zilizojengwa na serikali zikiwa na zaidi ya wanafunzi 10,000. Wakati serikali ilizitambua kuwa wadi, ilifahamu kuwa haikuwa sehemu ya msitu,” akasema Bw Murkomen ambaye ni Seneta wa Kaunti ya Elgeyo Marakwet.

Itakumbukwa kuwa, mnamo 2013 siasa zilizogubika suala zima la utunzaji wa msitu wa Mau zilimgharimu kisiasa kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga.

Katika uchaguzi mkuu wa 2007, wakazi wa eneo hilo walimuunga mkono Bw Odinga katika kinyang’anyiro cha urais.

Lakini Bw Odinga alipoongoza mpango wa utunzaji wa msitu wa Mau alipohudumu kama Waziri Mkuu katika serikali ya muungano, wanasiasa wa Rift Valley wakiongozwa na Dkt Ruto, wakati huo, walipinga mpango huo. Ndio maana Bw Odinga alipoteza ushawishi wa kisiasa katika eneo hilo na kumwathiri katika uchaguzi uliofuatia.

Kujenga upinzani

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema, mpango wa serikali wa kutekeleza awamu ya pili ya ufurushaji wa watu wanaoishi msitu wa Mau huenda ukajenga upinzani mwingine katika eneo hilo dhidi ya Dkt Ruto.

“Suala la uhifadhi wa msitu wa Mau na kufurushwa kwa familia zinazoishi katika chemichemi hii ya maji huenda ukazaa vuguvugu lingine la kumchapa Ruto kisiasa katika eneo hili ambako ana ufuasi mkubwa. Hii bila shaka itaathiri safari yake ya kuingia Ikulu 2022,” asema mchanganuzi wa siasa Herman Manyora ambaye ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Akaongeza: “Kile kilichomfika Raila 2013 kuhusiana na suala hili la Mau huenda kikampata Dkt Ruto endapo ataonekana kuunga mkono hatua ya serikali au ikiwa ataamua kunyamaza. Watu hawa watamtarajia kupinga mpango huu alivyofanya 2013.”

Kwa upande wake, mdadisi wa siasa, Bw Martin Andati anasema ni wazi kuwa Dkt Ruto sasa amejipata katika njia panda kuhusiana na suala zima la uhifadhi wa msitu wa Mau kwa sababu unaendeshwa na serikali ambayo anahudumia.

“Waziri wa Mazingira na Mali Asili Keriako Tobiko na Mshirikishi wa Ukanda wa Rift Valley George Natembeya wameapa kwamba awamu ya pili ya ufurushaji wa familia zinazoishi katika Msitu wa Mau sharti uendelee. Na kwa kuwa wawili hao wanaongoza serikali ambayo Dkt Ruto anahudumia, hatakuwa na lingine ila kuunga mkono mpango huo,” anasema.

Mapema mwaka huu, Dkt Ruto alisema serikali itaendelea na mpango wake wa kuhifadhi misitu yote nchini ikiwemo Mau. Akiongea katika wadi ya Sagoo katika eneo bunge la Narok Kusini, Naibu Rais alifafanua kuwa ni wale ambao wamevuka mpaka uliowekwa na kuingia ndani ya msitu wa Mau ndio wataondolewa lakini bila kutumia “nguvu kupita kiasi”.

Katika awamu ya kwanza iliotekelezwa mwaka jana, jumla ya familia 10,000 zilifurushwa kutoka wadi ya Reiyan kwa nguvu hali ambayo iliibua kero kuu kutoka kwa wabunge wa Rift Valley.