Habari MsetoSiasa

Mau: Murkomen awakaripia Tobiko na Natembeya

September 4th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Wengi katika Seneti Kipchumba Murkomen amemsuta Waziri wa Mazingira Keriako Tobiko kwa kuendeleza kuamuru kufurushwa kwa watu kutoka msitu wa Mau bila kupata idhini kutoka kwa Baraza la Mawaziri.

Kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge Jumatano Bw Murkomen alidai Rais Uhuru Kenyatta hajatoa amri kama hiyo akisema ufurushaji huo unapangwa na watu “wenye nia ya kugawanya Wakenya kwa misingi ya kisiasa kwa kutumia Mau kama kisingizio.”

“Ukweli ni kwamba serikali ya Kenya inayoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta haijawasilisha mbele ya baraza la mawaziri uamuzi kuhusu namna ya kuwapa makao mapya wakazi wa Mau. Ukweli ni kwamba baraza la mawaziri halijatoa uamuzi kama huo na serikali ya Jubilee haiko tayari kuwafurusha watu wake. Huu ni uamuzi uliofanywa na Waziri mmoja na Kamishna wa Kanda ambao wanataka kukiuka sheria,” akasema Murkomen.

Seneta huyo wa Elgeyo Marakwet pia aliwakashifu viongozi wengine wa kisiasa ambao, alisema, wanatumia mzozo huo wa Mau kuwaharibia sifa Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto.

“Rais Uhuru Kenyatta ni rais wa Wakenya wote, makabila yote na jamii zote. Naibu wake pia ni Naibu Rais wa Jamhuri ya Kenyatta wala sio jamii ya Kalenjin. Kwa hivyo hawa watu wajue kuwa serikali ya Kenya inaelewa njama zao za kisiasa,” Bw Murkomen akasema.