Akili Mali

Maua ya pesa yanayofanya wakulima kufyeka chini majanichai

May 13th, 2024 3 min read

NA LABAAN SHABAAN

JUA linazama na kumwaya miale yake katika mashamba ya pareto yanayometameta Wadi ya Merigi, Bomet Mashariki.

Maua meupe yanayongayonga kwenye upepo, yakiakisi matumaini ambayo wakulima wadogo wanayo kwa mmea huu.

Tukiandamana na afisa wa kilimo wa kaunti Joan Cherotich, kikosi cha Akilimali kina hamu ya kujua kwa nini mashamba yanayokuza pareto yanaongezeka.

Mvua inayonyesha maeneo hayo ni kichocheo kikubwa cha kunawiri kwa mazao haya.

“Inafaa tutembee haraka kwa sababu kunaweza kunyesha wakati wowote,” Cherotich alionya akituelekeza katika shamba moja la maua.

Ndiyo, mvua ya kutosha inayoshuhudiwa katika milima hii imewafaa wakulima.

“Natumai mnahisi anga baridi hapa,” Cherotich akauliza. “Hali hii ya hewa ni muhimu sana kwa ukuzaji pareto.”

Bomet ni miongoni mwa kaunti zinazostawi katika uzalishaji wa pareto – mmea unaotengeneza dawa ya kuua wadudu.

Walitema Mimea Mingine Ili Kukuza Pareto

Stanley Kiplangat aonyesha maua ya pareto aliyovuna shambani mwake. PICHA | LABAAN SHABAAN

Mercy Chepkemoi ni mmoja wa wakulima waliofana katika kilimo cha pareto. Aliacha kulima majani chai mwaka wa 2018 na hajawahi kuangalia nyuma.

“Nilisikia kuhusu kilimo cha pareto mwaka wa 2018 na nikapiga moyo konde kuikuza,” Chepkemoi alifunguka.

“Nilipigwa jeki na kampuni ya kuchakata pareto ya Kentegra Biotechnology ambayo ilinitengenezea kivungulio (greenhouse), ikanipa mafunzo na pia kunisaidia kupata miche,” aliongeza.

Ziara ya mara kwa mara ya Cherotich mashambani humu imeinua matumaini ya wakulima.

“Wakulima wengi wana hamu ya kukuza pareto kwa sababu ya msaada wanaopokea kupitia mipango ya serikali na usambazaji wa miche mizuri,” Cherotich alisema.

Chepkemoi anaeleza kuwa ardhi yake ya thuluthi ya ekari anayokuzia pareto imemboreshea mapato.

“Bei ya kilo moja ya maua yaliyokaushwa imekuwa ikipanda tangu nilipoanza upanzi. Mwanzoni, ilikuwa Sh200 na sasa tunauza kwa Sh310,” anafichua.

Mkabala na shamba la Chepkemoi, kuna kipande cha ekari moja cha Stanley Kiplangat anachotumia kukuza pareto. Kiplangat alitema viazi mnamo 2018 na kukumbatia pareto.

“Mimi hujikimu kutoka kwa mapato ya pareto. Serikali ya kaunti hutuma wataalamu ili kutuonyesha njia bora za kuzalisha pareto,” anadokeza.

Mnamo 2021, mashamba ya Bomet yalizalisha takriban kilogramu 3,260 za maua makavu yalipokewa na Kampuni ya Kusindika Pareto Kenya (PPCK) na Kentegra.

Haya ni kulingana na ripoti ya Mamlaka ya Kilimo na Chakula (AFA) ambayo imenakili kuwa idadi kubwa ya wakulima wamekumbatia kilimo cha pareto katika kaunti 18.

Zao hili hukuzwa katika kaunti za Meru, Nyandarua, Nyeri, Kiambu, Trans Nzoia, Uasin Gishu, Bungoma, Pokot Magharibi, Elgeyo Marakwet, Nandi, Baringo, Laikipia, Nakuru, Narok, Kericho, Bomet, Kisii na Nyamira.

Ukuzaji Pareto Unafufuka

Mtaalamu wa kilimo Joan Cherotich katika kivungulio cha kukaushia mazao ya pareto. PICHA | LABAAN SHABAAN

Kadhalika, AFA inaripoti kuwa tani 501 zilichakatwa nchini Kenya 2021, ikilinganishwa na tani 284 zilizosindikwa mwaka wa 2020.

“Takriban asilimia 98 ya bidhaa za pareto zinauzwa nchi za nje,” ripoti ya AFA inaweka wazi. Kenya huuza mazao ya pareto katika nchi zilizo bara Ulaya, Asia na Amerika.

Mintarafu hii, sekta ya pareto iko katika nafasi nzuri ya kuongeza mapato kutoka nchi za nje, kuvumisha ustawi wa viwanda na kukuza ukuaji wa uchumi.

Kwa mujibu wa AFA, mpango wa ufufuaji wa sekta hii unashughulikia changamoto za uzalishaji, masoko, teknolojia, usimamizi na kadhalika.

Moja ya sababu kuu za serikali kufufua pareto ni kupunguza umaskini katika maeneo ya mashambani nchini.

AFA inasema kwa sasa  uzalishaji na uchakataji wa maua makavu kwa mwaka ni wa thamani ya Sh395 milioni.  Hili ni ongezeko la asilimia 130 kati ya 2017 na 2021.

Itakumbukwa kwamba Kenya ilikuwa nchi iliyoongoza kwa uzalishaji wa pareto duniani. Nchi hii ilikuwa inakuza takriban asilimia 70 ya mazao yaliyofikishwa sokoni baada ya kuanza kilimo chake mwaka wa 1928.

Kenya iliwahi kuvunja rekodi kwa kuzalisha tani 17,710 za pareto iliyokaushwa mwaka wa 1992-93. Sehemu kubwa ya mazao haya ilitoka kwa wakulima wadogo.

Baada ya Kenya kuyumbayumba, China, Australia, Uganda, Tanzania, na Rwanda zilimega sehemu kubwa ya soko la Kenya.

Sababu kadhaa zilichangia kudorora kwa uzalishaji wa maua haya zikiwa ni pamoja na ushindani na changamoto za kufikia masoko.

Licha ya kuzalisha pareto ya hali ya juu, Kenya ilikuwa na matatizo ya uuzaji na usindikaji. Bodi ya Pareto ya Kenya (PBK) ilikuwa kampuni ya kipekee ambayo ilikuwa inachakata pareto. Baadaye ilianza kushindwa kuwalipa wakulima waliowasilisha maua.

Sheria yapisha soko huru

Sheria ya Mimea ya 2013, ilifungua mwanya wa mageuzi ambayo yalifungua wigo wa soko.

Sasa wachakataji wa pareto wameongezeka na hakuna ukiritimba wa kutegemea mchakataji mmoja.

Baadhi ya mashirika ambayo yanapokea maua ni Pyrethrum Processing Company of Kenya (PPCK), Botanical Extracts Export Processing Zone, Africhem Botanicals Ltd, Kentegra Biotechnology, na Highchem East Africa

Kenya inatarajia kuzalisha na kusindika hadi tani 20,000 za pareto na kupata Sh7.5 bilioni kutokana na mauzo ya bidhaa kwa mwaka siku za usoni.