Habari za Kitaifa

Mauaji: Kawira asisitiza ukweli utabainika, uongo uyoyomee gizani

January 16th, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

GAVANA wa Kaunti ya Meru Kawira Mwangaza  amesisitiza kuwa ukweli utabainika kuhusu chanzo halisi cha kifo cha bloga Daniel Muthiani almaarufu kama ‘Sniper’, baada ya mumewe kuhojiwa na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI).

Mumewe gavana huyo, Bw Murega Baichu na dadake, Miriam Guantai, walihojiwa na DCI mnamo Jumatatu kuhusiana na kifo cha mwanablogu huyo mjini Meru.

“Nimebaki mtulivu katikati mwa dhoruba. Uongo unaweza kusambaa kote duniani wakati ukweli haujatokea, ukiwa bado unavaa viatu. Tutashinda kwa neema ya Mungu!” akasema Bi Mwangaza.

Polisi walisema kuwa Bw Baichu aliagizwa kufika kwao na kuhojiwa kwa saa kadhaa Jumatatu, katika afisi ya DCI mjini Meru.

Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi zinazoendelea kubaini chanzo cha mauaji hayo.

Bw Baichu alikuwa ameandamana na mawakili wake alipofika mbele ya maafisa wanaochunguza kisa hicho, ambacho kimezua hisia kali katika eneo hilo.

Mshirikishi Mkuu wa DCI katika eneo la Mashariki, Bw Lenny Kisaka, alithibitisha kuhojiwa kwa Bw Baichu, akiongeza kuwa uchunguzi kuhusu mauaji hayo unaendelea vizuri.

Haikubainika mara moja kuhusu maswali waliyoulizwa, japo duru ziliieleza ‘Taifa Leo’ kwamba kuhojiwa huko ni sehemu ya uchunguzi unaoendelea.

Kufikia sasa, jumla ya washukiwa wanane wanazuiliwa na polisi.

Kundi la makachero kutoka Nairobi, Meru na Embu wanachunguza kisa hicho.

Bi Mwangaza amekanusha kufahamu lolote kuhusu mauaji hayo huku akishinikiza uchunguzi huo kuendeshwa kwa uwazi na njia ya haki.

Mnamo Ijumaa wiki iliyopita, upande wa mashtaka uliiomba Mahakama Kuu ya Kiambu kuruhusu washukiwa watano wanaohusishwa na mauaji hayo kuendelea kuzuiliwa kwa siku 14 zaidi, ili kuwapa polisi muda wa kutosha wa kufanya uchunguzi wao.

Upande wa mashtaka unawataka Kenneth Mutua, Fredrick Muruiki, Franklin Kimathi, Timothy Kinoti na Murangiri Kenneth Guantai kuendelea kuzuiliwa na polisi uchunguzi huo ukiendelea.

Wanakabiliwa na mashtaka ya mauaji kinyume cha Sehemu 203 na 204 ya Sheria za Kukabiliana na Uhalifu za Kenya.

Mwanablogu huyo, 33, aliuawa mnamo Desemba 16, 2023.

Kupitia wakili Evelyn Onunga, upande wa mashtaka ulisema kuwa kuwaachilia washukiwa hao watano kutavuruga shughuli za uchunguzi unaoendelea. Upande huo ulisema pia huenda wakaingilia au kutoa vitisho kwa mashahidi.

Washukiwa walikamatwa mjini Meru na makachero na kupelekwa katka vituo tofauti vya polisi Kiambu na Nairobi mnamo Januari 4, 2024.