Habari MsetoSiasa

MAUAJI KIAMBAA: Ruto aelezea kanisa lilivyoleta amani baada ya machafuko

July 31st, 2018 2 min read

Na VALENTINE OBARA

NAIBU Rais William Ruto, Jumatatu aliibua kumbukumbu za mauaji yaliyotokea katika Kanisa la Kenya Assemblies of God (KAG), eneo la Kiambaa, Kaunti ya Uasin Gishu wakati wa ghasia za baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2007.

Kisa hicho ambapo watu 35 waliteketea walipokuwa wamejificha ndani ya kanisa kilikuwa miongoni mwa matukio ya kikatili zaidi kuwahi kushuhudiwa katika kipindi hicho, na mojawapo ya visa vilivyodaiwa kuchochewa na Bw Ruto na mwanahabari Joshua Sang katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

Akihutubia waombolezaji wakati wa ibada ya wafu ya marehemu Dkt Peter Njiri ambaye alikuwa Chansela wa Chuo Kikuu cha KAG East kilicho Kitengela, Bw Ruto alieleza jinsi kanisa hilo lilivyojitolea kuleta amani nchini baada ya kisa hicho cha kutisha.

“Kutokana na matukio ya 2007/2008, ni juhudi za viongozi wa kidini wakiongozwa na Peter Njiri ambazo zilitusaidia kupata msingi mpya wa kisasa katika nchi yetu. KAG iliathiriwa pakubwa na matukio hayo,” akasema katika ukumbi wa chuo hicho.

Kesi zote kuhusu ghasia za baada ya uchaguzi zilisitishwa baada ya Kiongozi wa Mashtaka katika mahakama ya ICC, Bi Fatou Bensouda, kuambia mahakama hiyo kwamba hapakuwa na ushahidi wa kutosha kuthibitisha washukiwa walikuwa na hatia.

Naibu Rais alisema viongozi wa makanisa walikuwa katika mstari wa mbele kuleta upatanisho kati yake na Rais Uhuru Kenyatta kabla Uchaguzi Mkuu wa 2013, kama njia mojawapo ya kuondoa uhasama uliosababisha vita vibaya zaidi vya kijamii kuwahi kushuhudiwa nchini baada ya uchaguzi wa 2007.

“Ni kwa sababu ya jinsi kanisa na viongozi wa kidini walivyojitolea kwa maombi ambapo Rais Uhuru Kenyatta, mimi na wengine wengi tulipata msingi mpya wa kisiasa usiotegemea chuki, ukabila na mgawanyiko wa kijamii,” akasema.

Aliongeza: “Tulichukua msimamo na tunaamini kwamba hakutawahi kushuhudiwa tena umwagikaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia wala uharibifu wa mali na makanisa kwa sababu ya ushindani wa kisiasa.”

Kando na hayo, Bw Ruto aliwasilisha risala za rambirambi kwa jamaa na marafiki wa Dkt Njiri kutoka kwa Rais ambaye asingeweza kuhudhuria ibada hiyo.

Alitoa wito kwa kanisa kushirikiana na serikali ili kufanikisha malengo ya kuleta maendeleo yatakayoboresha maisha ya wananchi wote kitaifa.

Alisema kanisa limekuwa mshirika mkubwa wa serikali kwa miaka mingi katika sekta mbalimbali kama vile afya na elimu. Uboreshaji wa afya ni moja ya malengo manne makuu ya Serikali ya Jubilee.

“Tuna historia ya kushirikiana na kanisa. Tuna imani kwa kanisa na serikali imejitolea kustawisha ushirikiano huo. Tungependa kushirikiana na kanisa na tungependa kushirikiana na KAG. Nina matumaini kwamba mtakubali kushirikiana nasi,” akasema.

Dkt Njiri ambaye pia alikuwa Mwenyekitii wa Shirikisho la KAG ukanda wa Afrika Mashariki alifariki Julai 17, na mazishi yake yalifanywa katika boma lake lililo Milimani, Kitengela.