Habari Mseto

Mauaji ya mwanafunzi Kibra yachunguzwa

December 27th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

INSPEKTA Mkuu wa Polisi, Joseph Boinnet, ameagiza kuchunguzwa kwa mauaji ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Leeds nchini Uingereza, Carilton David Maina.

Marehemu, aliyekuwa na umri wa miaka 23, anasemekana kupigwa risasi na afisa wa polisi mnamo Ijumaa wiki jana akitoka dukani kununua filamu katika mtaa wa Kibera Line Saba.

“Tungependa kujulisha umma kuwa Inspekta Mkuu wa Polisi ameomba Mamlaka ya Uangalizi wa Utendakazi wa Polisi (IPOA) kufanya uchunguzi wa dharura kuhusiana na kisa cha mauaji mtaani Kibera, ambapo Carilton Maina aliuawa,” ulisema ujumbe kutoka kwa afisi ya Bw Boinnet.

IPOA ilisema imeanzisha uchunguzi na itatoa mapendekezo kuhusiana na hatua za kinidhamu dhidi ya afisa aliyehusika katika kumuua Maina baada ya kumaliza uchunguzi.

Mwanafunzi huyo alikuwa katika likizo na alitarajiwa kurejea Uingereza hapo Januari 2019 ili kuendelea na masomo yake.

Kulingana na shirika la kutetea haki za kibinadamu la Amnesty International, mauaji ya Maina yalikuwa ya kiholela kwani hakuwa jambazi kama walivyodai polisi.

“Kulingana na ushahidi wa wakazi, Maina hakuwa na rekodi ya ujambazi. Alikuwa amefanya vyema maishani hasa katika spoti na elimu,” ilisema taarifa ya Amnesty na kuongeza kuwa mwendazake alisomea katika Shule ya Upili Brookhouse baada ya kupata ufadhili, kabla ya kujiunga na Leeds University kusomea uhandisi.

Shirika hilo limetaka polisi kumpokonya bunduki afisa aliyehusikaili iweze kuchunguzwa, na kuongeza kuwa zaidi ya visa 180 vya mauaji ya kiholela yaliyohusisha polisi yameripotiwa nchini mwaka huu.

Maafisa 10 wa polisi wamepatikana na makosa katika mauaji ya aina hiyo, na matumizi mabaya ya mamlaka.

Mnamo Februari 7 mwaka huu, Jaji James Wakiaga alimhukumu Titus Musila, almaarufu Katitu, miaka 15 jela kwa kupatikana na makosa ya kumuua mshukiwa, Kenneth Kimani mnamo 2013.

Naye aliyekuwa mkuu wa kituo cha polisi cha Ruaraka, Nahashon Mutua, alipatikana na makosa ya kumuua Martin Koome alipokuwa amezuiliwa seli kwa madai ya kupigana na mkewe.