HabariSiasa

MAUAJI YA SHARON: DPP tayari kunasa Gavana Obado

September 10th, 2018 2 min read

NA WAANDISHI WETU

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP), Noordin Haji Jumapili alisema yuko tayari kumkamata Gavana wa Migori, Okoth Obado iwapo uchunguzi unaoendelea utamhusisha na mauaji ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Rongo, Sharon Otieno.

Bw Haji alisema kuwa, sheria haitaacha mtu yeyote nje hata awe ni wa ngazi ya juu vipi iwapo uchunguzi utapendekeza ashtakiwa kwa mauaji hayo ya kinyama wiki iliyopita.

“Kitu kimoja ambacho ninataka kuwahakikishia ni kuwa hakuna yeyote ambaye ataachwa. iwapo wewe ni gavana ama la, ni lazima utakabiliwa na sheria. Uchunguzi bado unaendelea lakini wakati mwafaka ukiwadia na tukiona haja ya kukamatwa kwa gavana huyo, basi atakamatwa tu,” alisema Bw Haji alipoulizwa iwapo Bw Obado atakamatwa.

Akizungumza kwa mara ya kwanza tangu uchunguzi wa mauaji ya Bi Otieno, ambaye alitekwa nyara akiwa na mwanahabari wa shirika la Nation Media Barrack Oduor ulipoanza, Bw Haji alisema kuwa afisi yake inafuatilia suala hilo kwa makini ili kuhakikisha kuwa sheria inafuatwa.

“Kile tu ambacho ningetaka kuomba umma ni tupeane muda mwafaka kwa maafisa wetu wa uchunguzi wamalize kazi yao. Maafisa wetu wanasaidiana na maafisa wa uchunguzi ipasavyo,” alisema Bw Haji wakati wa kikao na wanahabari katika afisi za shirika la kutetetea haki za binadamu la Haki Africa jijini Mombasa.

Wakati huo huo, Bw Haji alisema kuwa uchunguzi utafanywa kubaini jinsi afisa anayesemakana kutoka kitengo cha ujasusi cha jeshi alivyoingia katika seli na kumuona msaidizi wa Bw Obado, Bw Michael Oyamo, ambaye ndiye mshukiwa pekee anayezuiliwa kuhusiana na kifo cha Sharon.

Maswali yameulizwa kuhusu sababu ya afisa huyo, ambaye Taifa Leo imegundua kuwa ni afisa wa ujasusi wa jeshi, kumtembelea Bw Oyamo.

“Hata kama mshukiwa ana haki ya kutembelewa akiwa jela kulingana na sheria, maswali ambayo tunatataka yajibiwe baada ya uchunguzi huu ni iwapo ziara ya afisa huyo ilifanyika kisheria,” alisema Bw Haji ambaye alikuwa ameandamana na mkurugenzi mkuu wa shirika la Haki Africa, Hussein Khalid.

Jana, afisa huyo aliyetambuliwa kama Lukas Ouko alisisitza kuwa anafanya kazi na kitengo cha ujasusi cha jeshi la wanamaji na alitumwa rasmi kumtembelea Bw Oyamo.

“Mimi ni raia mwema na sikuenda Migori kwa maslahi yangu ya kibinafsi,” afisa huyo aliambia Taifa Leo.

Alisema anahudumu katika kambi la wanajeshi wa majini iliyoko Mtongwe mjini Mombasa, na aliwapa maafisa wa polisi wa Homa Bay barua rasmi kutoka kwa jeshi ya kumruhusu kumuona Oyamo.

Hata hivyo, msemaji wa jeshi la Kenya Kanali Paul Njuguna alisema jeshi haikumtuma afisa yeyote kumuona Oyamo ambaye aliacha kazi ya jeshi.

Haya yanajiri huku Wabunge Waakilishi Wanawake eneo la Nyanza wakipanga maandamano makubwa kushinikiza haki kwa Sharon.

Viongozi hao Pamela Odhiambo (Migori), Janet Ong’era (Kisii), Rosa Buyu (Kisumu) na Gladys Wanga (Homa Bay) walisema maandamano hayo pia yatakuwa ya kutetea haki za wanawake wanaodhulumiwa.

Wanne hao walikuwa wametembea nyumbani kwa wazazi wa marehemu Sharon.

“Tunawaomba maafisa wa DCI kuharakisha uchunguzi. Washukiwa wakuu wanajulikana,” akasema Bi Wanga.

Mwito huo wa maandamano pia uliungwa mkono na mwenyekiti wa ODM, John Mbadi.

Wanafunzi wa kike wa Chuo Kikuu cha Rongo pia wamepanga kushiriki maandamano hayo.

Wabunge kutoka eneo la Kisii na Nyamira pia walishtumu vikali mauaji hayo. Waliojitokeza kulaumu ni Ezekiel Machogu (Nyaribari Masaba), Alfa Miruka (Bomachoge Chache), Richard Tongi (Nyaribari Chache), Ben Momanyi (Borabu), Joash Nyamoko (North Mugirango) na Shadrack Mose (Kitutu Masaba).

Taarifa za Mohamed Ahmed, Justus Ochieng, Vivere Nandiemo na Magati Obebo