Habari za Kitaifa

Mauaji ya Sniper: Gari lililotumika kutupa mwili lapatikana

January 27th, 2024 1 min read

NA LABAAN SHABAAN

GARI lililotumika katika utekaji nyara na kisha utupaji wa mwili wa bloga David Muthiani almaarufu Sniper limepatikana eneo la Kithoka, Kaunti ya Meru, Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) imefichua.

Sniper alitekwa nyara na kuuawa kisha mwili wake kutupwa mtoni Mutonga eneo la Chiakariga, Kaunti ya Tharaka Nithi mnamo Desemba 2, 2023.

“Utambuzi na kupatikana kwa motokaa aina ya Toyota Premio yenye nambari ya usajili KCR 742N ulijiri baada ya uchunguzi wa makini wa kijasusi kutumia vidokezo muhimu,” ilisema DCI katika mtandao wa X (zamani Twitter) mnamo Jumamosi.

DCI inaripoti kuwa gari hilo la fedha lilipatikana eneo la Canopy, Meru.

Makachero wanaopeleleza kiini na wahusika wa kifo hiki wamemtambua mshukiwa Vincent Mureithi Kirimi almaarufu Supuu kuwa dereva aliyekodi gari hilo siku ya utekaji nyara na kuuawa kwa Sniper.

Kulingana na DCI, gari hilo liliwabeba Brian Mwenda, Christus Manyara Kiambi, na Bonface Kithinji Njihia almaarufu DJ Kaboom.

Upelelezi zaidi unaendelea majasusi wakishinikizwa na umma pamoja na viongozi wa kisiasa kuharakisha mchakato wa kesi na washukiwa kufungwa.