Mauaji ya Wakenya kiholela yazidi miili 19 ikipatikana Mto Yala

Mauaji ya Wakenya kiholela yazidi miili 19 ikipatikana Mto Yala

NA WAANDISHI WETU

KUZOROTA kwa hali ya usalama nchini kumefikia kiwango hatari hasa kutokana na ongezeko la visa vya watu kutoweka kisha kupatikana wameuawa.

Kisa cha majuzi ni kupatikana kwa miili 19 ya watu waliouawa ikiwe imetupwa ndani ya Mto Yala, Kaunti ya Siaya.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yakiongozwa na Haki Afrika yanawalaumu polisi kwa madai kuwa ndio wahusika wakuu wa mauaji ya raia.

Mkurugenzi mkuu wa Haki Afrika, Hussein Khalid alisema visa vya watu kutoweka na miili yao kutupwa mitoni ama misituni vimesambaa kote nchini.

Kamanda wa polisi eneo la Gem, Charles Chacha alithibitisha kuwepo kwa ongezeko la miili inayoopolewa Mto Yala.

Katika mochari ya hospitali ya Yala Sub-County katika eneobunge la Gem kuna miili 20 ya watu wasiojulikana, ambapo 19 kati ya hiyo iliopolewa kutoka Mto Yala, saba kati ya hiyo wiki iliyopita karibu na maporomoko ya Ndanu.

Afisa Mkuu wa Matibabu katika hospitali hiyo, Dkt Bruno Okal alisema miili hiyo imekuwa ikipelekwa katika mochari kwa muda wa miezi mitatu iliyopita, 19 kati ya hiyo ikipelekwa na polisi baada ya kuopolewa kutoka Mto Yala.

Dkt Okal alisema watazika miili hiyo katika kaburi la pamoja kwa kuwa hakuna jamaa waliojitokeza kuitambua na kuichukua. Kutotambuliwa kwa miili hiyo kunaonyesha kuwa waathiriwa wanatoke nje ya eneo hilo.

Mkazi mmoja aliambia Taifa Leo kuwa tangu Julai mwaka jana wakazi wamesaidiana na polisi kuopoa miili 31 ndani ya mto huo, ambapo mingi huwa kwenye magunia.

Wakazi wengine walisema kuwa miili hiyo huletwa kwa gari aina ya pick-up nyeusi na mara nyingine kwa Probox usiku wa manane ama alfajiri.

  • Tags

You can share this post!

Mdalasini na faida zake mwilini

Raila na Ruto wazidi kulisha Wakenya ahadi hewa

T L