Kimataifa

Mauaji ya Wapalestina 100 yaibua hisia kali duniani kote

Na Na MASHIRIKA August 10th, 2024 1 min read

ZAIDI ya Wapalestina 100 waliuawa na wengine  wengi wakajeruhiwa katika shambulio baya zaidi lililotekelezwa na Israel katika shule moja inayotumika kama hifadhi kwa watu waliopoteza makwao Ukanda wa Gaza, utawala wa Hamas ulisema Jumamosi.
Jeshi la Israel lilisema shambulio hilo la angani, lililotekelezwa usiku wa kuamkia jana, lililenga kituo cha kushirikisha shughuli za wapiganaji wa Hamas.
Shambulio hilo lilitekelezwa wakati watu wanaoishi katika shule hiyo walikuwa wakishiriki maombi ya alfajiri, kitengo cha kupeperusha habari za Hamas kikasema kwenye taarifa.
Idara ya Afya katika Ukanda wa Gaza haikutoa maelezo zaidi kuhusu shambulio hilo.
Jeshi la Israel lilisema katika taarifa kwamba, wanajeshi wake wa angani walilenga kituo kimoja cha kutoa maagizo kwa wapiganaji wa Hamas ambako baadhi yao walikuwa wakijificha.
 Jeshi hilo lilisema lilichukua hatua mwafaka kupunguza uwezekano wa kuwajeruhi raia “ikiwemo uchunguzi wa angani na ukusanyaji wa habari za kijasusi”.