Habari

Mauti, hasara zashuhudiwa kutokana na mvua kubwa

October 11th, 2019 2 min read

Na WAANDISHI WETU

MAAFA na uharibifu wa mali yalishuhudiwa Alhamisi baada ya mvua kubwa kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini tangu Jumatano usiku.

Maafa makubwa zaidi yalishuhudiwa katika Kaunti ya Meru ambako watu watano walipoteza maisha kwenye visa tofauti katika Kaunti ya Meru.

Katika kisa cha kwanza, watu watatu walisombwa na mafuriko katika soko la Naari walipokuwa wamejikinga mvua kanisani.

Mafuriko yaliyokuwa yakivuma yalibomoa mlango wa Kanisa la Hossana na kumsomba mtoto Boniface Muriungi ambaye alikuwa mwanafunzi wa shule ya St Augustine, Bi Muko Kinya na Bw James Karani.

Watatu hao walibebwa na maji hayo umbali wa karibu mita 400 kwenye barabara iliyojaa mawe.

Miili yao iliyokuwa na majeraha mabaya ilipatikana na wakazi alfajiri ikiwa imekwama kwenye mizizi ya miti.

Katika kijiji cha Karegia, Kaunti Ndogo ya Imenti Kaskazini, polisi walipata mwili wa Wilfred Mwirigi, 42, ambaye pia alisombwa na mafuriko.

Kijijini Kienderu, wakazi walishtuka walipopata mwili wa mwanamume asiyejulikana ambaye alipigwa na stima wakati mvua ilipokuwa ikinyesha.

Katika Kaunti ya Siaya, wanafunzi watatu walifariki wakati mgodi wa dhahabu ulipoporomoka na kuwafunika walipokuwa wakitafuta dhahabu Alhamisi asubuhi katika eneo la Nango, Bondo.

Miongoni mwa waliofariki ni David Ochieng Duro ambaye ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Egerton bewa la Nakuru, Nicholas Arwa ambaye alikuwa akisubiri kufanya Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Upili (KCSE) mwaka huu, na Kevin Ochieng’ Juma ambaye pia ni mwanafunzi wa shule ya upili.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Bondo, Bw Antony Wafula alisema miili ya watatu hao ilitolewa na kupelekwa katika hifadhi ya maiti ya Hospitali ya Rufaa Kaunti Ndogo ya Bondo.

“Migodi katika eneo hili itafungwa hadi mahitaji yote ya kiusalama yaafikiwe,” akasema Bw Wafula.

Mashamba

Katika Kaunti ya Murang’a, maporomoko ya ardhi yaliharibu mashamba ya majanichai katika kijiji cha Kairo, Kaunti Ndogo ya Mathioya.

Miti ya majani chai iling’olewa kutoka kwenye mashamba kadhaa na kusongezwa hadi katika mashamba jirani.

Mkurugenzi wa Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa katika eneo hilo, Bw Paul Murage alisema mvua iliyonyesha ilikuwa kubwa mno ndiposa kukatokea maporomoko hayo.

Alionya kwamba kuna uwezekano hali ikaendelea kuwa hivyo katika kaunti hiyo kwa siku zijazo.

Katika Kaunti ya Makueni, lori la kusafirisha mchanga lilisombwa na mafuriko katika Mto Tiva.

 

Taarifa za Dickens Wasonga, Charles Wanyoro, Ndung’u Gachane, na Pius Maundu