MAUYA OMAUYA: Bobi Wine ameweka msingi, mapambazuko yanakaribia

MAUYA OMAUYA: Bobi Wine ameweka msingi, mapambazuko yanakaribia

Na MAUYA OMAUYA

Ikiwa ulizaliwa mnamo 1986 nchini Uganda, basi kwa jumla ya miaka 35 umeishi chini ya utawala wa rais mmoja tu – Yoweri Kaguta Museveni.

La kutamausha ni kwamba utasubiri miaka sita zaidi kabla kupata fursa nyingine ya kubadili mkondo wa taifa lako.Wafaransa wana msemo kutokana na historia yao ya wafalme, “L’etat c’est moi” – yaani “Taifa ni mimi na mimi ndio taifa”.

Hali ilivyo nchini Uganda, sikutaraji matokeo tofauti kwenye uchaguzi wa urais uliofanywa juma lililopita. Rais Museveni ni katili aliyeteka nyara taasisi zote za serikali na nchi; amelewa chakari mamlaka na kujipumbaza kwamba yeye ndiye mkombozi wa taifa hilo, eti bila Museveni ikulu ya Nakasero, nchi itasambaratika.

Kwa muda mrefu, raia wa Uganda wamepotoshwa kwamba walikuwa katika hali mbaya sana kabla ya jeshi la NRA, chini ya Museveni, kutwaa utawala mwaka wa 1986.

Pia, wamelishwa propaganda eti mambo yatavurugika zaidi bila ‘mkombozi’ huyu usukani, eti hajakamilisha safari yake ya kuboresha nchi.Sio mara ya kwanza kwa raia wa Afrika kuingia mtego huu wa ‘mkombozi bandia’ na kisha kukandamizwa na mateso ya dikteka ambaye msukumo wake mkuu ni ubinafsi, tamaa ya ukuu na kuabudiwa.

Robert Mugabe wa Zimbabwe na Muammar Gaddafi wa Libya walikuwa na gonjwa lilo hilo la kujihisi ‘mkombozi’ wa mataifa yao. Wakaishia kuleta hasara ya kudumu kw nchi zao.Simulizi za ukombozi wa 1986 hazina maana kwa taifa baada ya miongo mitatu na zaidi.

Hazileti matumaini kwa vijana waliozama kwenye bahari ya vileo kwa kukosa ajira. Simulizi hizi ni ngano za upuzi kwa familia zinazoozea katika lindi la ufukara kwenye mitaa ya mabanda mjini Kampala au waliosahaulika vichakani Gulu kaskazini.

Ndiposa ni muhimu kuweka matumaini katika mwongozo wa Katiba, sio hekima ya mwanadamu. Tumeshuhudia jinsi katika muhula mmoja tu Donald Trump amechakiza na kudororesha ustaarabu wa demokrasia ya Amerika; sembuse Museveni nchini Uganda kwa miongo mitatu?

Ni bayana kwamba Rais Museveni hana nia ya kung’atuka mamlakani. Ni wazi pia kwamba hakuna jipya atawatendea raia kipindi hiki cha ukongwe wake kama hakutenda mapema.

Kwa hakika, matendo yake ya karibuni yanaashiria anazidisha ukatili dhidi ya wapinzani.Ikiwa tulishangazwa na aliyomtendea Kizza Besigye enzi zile, yaliyompata Bobi Wine yametuatua nyoyo.

Kadri miaka inavyosonga ndivyo dikteta huyo anavyozidisha ukatili.Kiongozi wa sampuli ya Museveni, Mugabe au Gaddafi hawezi kutimuliwa isipokuwa kwa aina ya mapinduzi. Amegeuka dude linaloongozwa na hofu ya kupoteza mamlaka na hana imani kwa raia anaowawakilisha.

Kupitia uchaguzi wa Januari 2021, Bobi Wine amefaulu kuwasha hisia za mwamko mpya katika mawazo ya vijana. Ameamsha hasira ya taifa lililohadaiwa, ameweka msingi wA miereka ijayo.

Hasira ya halaiki ni kiungo muhimu katika mapinduzi ya kuvunjavunja ngome za udikteta.Ikiwa mbinu iliyosalia kwa rais kuongoza taifa ni kupitia nguvu za risasi na jeshi, basi mapambazuko yako karibu.

Linalohitajika ni kusambaza ujasiri wa Bobi kote Uganda. Kiu ya mabadiliko ikisambaa kwa kila raia, Museveni hatadumu. Tayari Bobi Wine ameweka msingi WA miereka ijayo. Madhila, vifungo na vipigo alivyovipata Bobi ni dhihirisho kuwa nyani amefika jangwani, anachakura tu, pa kuegemea hakuna.

You can share this post!

BENSON MATHEKA: Museveni amegeuza Uganda kuwa mali ya...

FAUSTINE NGILA: Madikteta wasiruhusiwe kutumia mitandao...