MAUYA OMAUYA: Usitarajie mabadiliko Kenya mwaka huu

MAUYA OMAUYA: Usitarajie mabadiliko Kenya mwaka huu

Na MAUYA OMAUYA

TABIA moja ya ndege mbuni ambayo imesimuliwa vizazi kwa vizazi, ni kuficha kichwa chake mchangan anapokabiliwa na hatari ya adui.

Katika hali hiyo haoni adui, hivyo huamini ataepuka hatari. Ukweli ni kwamba, sehemu ya mwili iliyotiwa mavumbini ni kidogo mno, na maangamizi yakija humfagia kabisa.Ndivyo hali katika taifa letu.

Tusijipumbaze kuhusu utofauti ambao mwaka mpya 2021 utaleta. Maisha hayabadiliki kwa sababu kumekucha alfajiri au giza limetanda usiku. Jamii inayotegemea miujiza aina hii husalia katika tope la mazoea. Kila wakati maovu ya jana na leo yanapoendelea kuathiri kina yakhe, wao hupiga dua kuwa kesho italeta afueni, itakuwa?afadhali.

Mambo yanavyozidi kuvurugika wanaongeza sala na matumaini kwamba?mabadiliko ya majira yataleta mazuri. Ni muhimu kufahamu kuwa zaidi ya dua na matumaini, tunahitaji mikakati na jitihada kamili za kubadili hali.Mwaka 2020 ulikuwa wa giza totoro kwa kila Mkenya na ulimwengu mzima. Makali ya janga la virusi vya corona yametikisa kila pembe.

Hakuna kitu maishani hakijaathirika: afya, ajira, siasa, elimu, uchumi, familia, uchukuzi, kilimo, utalii.Linalosikitisha ni kuona taasisi za nchi zimezidi kuzorota; wananchi wamebakia kusubiri kwa imani?kwamba mabadiliko yatafika kwa ujio wa mwaka mpya.

Hii ni ndoto mbaya na Wakenya?watagundua hivi karibuni kwamba bila juhudi thabiti, madhila ya 2020 yataongezeka maradufu?mwaka huu wa 2021.Taifa haliwezi kustawi ikiwa maafa ya mwaka jana hayatuletei mafunzo na?mabadiliko ya kudumu.

Mfano halisi umedhihirika katika sekta ya afya na elimu. Yapata mwaka mzima baada ya janga kutua, serikali haina suluhu au mwafaka wowote thabiti kukabili migomo ya wahudumu wa afya au kuimarisha miundomsingi inayohitajika.

Hali kwenye zahanati vijijini ni mbaya hata zaidi sababu walaghai wametumia?janga la corona kuzamisha sekta zaidi.Yamkini viongozi sasa wamejitia hamnazo kwa imani kwamba chanjo ya corona itafika nchini hivi karibuni na balaa yote katika sekta ya afya itatokomea.Hali itakuwa vipi iwapo virusi vipya ibuka vya corona vitazagaa na kuongeza makali na kukaidi chanjo?

Tutakumbana tena na hali ile ile ya uozo kwenye hospitali zetu! Hii ina maana kwamba mwaka huu?huenda mambo yakazorota zaidi sababu hatujawekeza katika mikakati ya kujitayarisha kukabiliana na janga hilo.

Taifa pia litakumbana na balaa nyingine kubwa katika sekta ya elimu. Kwa miezi kumi, hatukujitayarisha kwa lolote, na tumegutuka tu hii Januari kwamba tunahitaji kufungua shule ilhali uwezo hatuna.

Shule za kibinafsi zimemezwa na janga huku za umma zikishindwa kumudu ongezeko la wanafunzi sababu ya ukosefu wa vifaa.Kama kawaida, taifa linasubiri muujiza wa mwaka mpya kutunasua. Ni mithili ya mbuni kutia kichwa mavumbini!

mauyaomauya@live.com

You can share this post!

BENSON MATHEKA: Wakenya wamechoshwa na undumakuwili wa...

Hofu ya wanavijiji kumiliki silaha kali Kapedo