Mauzo: Ngamia wachelewesha meli kuondoka bandarini Lamu

Mauzo: Ngamia wachelewesha meli kuondoka bandarini Lamu

Ni mwezi mmoja sasa tangu meli hiyo MV Banyas 1 kuwasili kwa mara ya pili katika bandari ya Lamu kuchukua mifugo wanaopelekwa ng’ambo.MV Banyas 1 ilitia nanga Novemba 5, 2022 na ilifaa kuanza safari ya kuelekea Oman baada ya majuma mawili.

Katika shehena yake ni takriban mifugo 7,000 wanaojumuisha ngamia 1,000, mafahali 300 na mbuzi na kondoo 6,000.

Meneja Msimamizi wa Mizigo Bandarini Lamu, Bw Peter Masinde, alisema changamoto za kuleta ngamia kutoka kaunti kama vile Wajir na Garissa hadi Lamu ndizo zimechelewesha safari.

Wenye ngamia wanalazimika kutembea na mifugo wao hadi Lamu kwani kuna wanakabiliwa na tatizo kuwabeba kwa malori.

Bw Masinde alieleza kuwa juhudi zinaendelea kuhakikisha idadi ya wanyama waliopangwa kusafirishwa katika awamu hii ya pili, inatimizwa wiki hii ili meli iondoke.

Meli ya MV Banyas 1 ikiwa imetia nanga bandarini Lamu. Meli hiyo ilifunga gati Novemba 5, 2022. PICHA | KALUME KAZUNGU

Kufikia Jumatatu, jumla ya ngamia 800, mafahali 580 na mbuzi na kondoo 3,000 tayari walikuwa wamefikishwa bandarini huku shughuli ya kuwapakia melini ikiendelea.

Biashara ya usafirishaji wa mifugo hadi mataifa ya nje kupitia bandari ya Lamu ilizinduliwa Oktoba 2022.

Shehena ya kwanza iliyoelekea Oman ilikuwa takriban mifugo 16,000 waliojumuisha mafahali 200 na mbuzi na kondoo 15,400.

Wakati wa safari hiyo, MV Banyas 1 ilisubiri bandarini Lamu kwa juma moja pekee.

Meli hiyo iliwasili Ijumaa, Oktoba 14, na kufikia Ijumaa iliyofuata, Oktoba 21, ilikuwa tayari imeng’oa nanga kuelekea nchini Oman.

Meneja wa mradi wa miundomsingi wa Lamu, maarufu Lapsset, katika ukanda wa Pwani, Bw Salim Bunu, jana alisema wafugaji wamepata afueni kwani awali walipata hasara tele kwa kukosa soko wa mifugo wao, walioishia kuangamizwa na kiangazi.

“Biashara inayoendelea ya mifugo imewainua wafugaji si Lamu pekee bali ukanda mzima wa kaskazini mwa Kenya,” akasema Bw Bunu.

  • Tags

You can share this post!

Gavana Achani alalamikia MCAs kuchelewa kuidhinisha...

Kaunti ya Kilifi yaweka mikakati ya kuwashughulikia...

T L