Habari

Mavazi ya Uhuru, Raila yaibua gumzo

October 21st, 2019 1 min read

Na WAANDISHI WETU

RAIS Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga waliibua mjadala Jumapili walipowasili wakiwa wamevaa mavazi yanayofanana katika sherehe za Mashujaa zilizofanywa Mombasa.

Bw Odinga, ambaye aliwasili wa kwanza, alikuwa amevaa mavazi meupe kutoka juu hadi chini na kofia.

Rais naye aliwasili wa mwisho akiwa amevaa shati nyeupe iliyofanana na ile ya Bw Odinga pamoja na kofia sawa na yake.

Baadhi ya Wakenya walidai hayo yanaonyesha ushirikiano mpya unaotarajiwa wakati ripoti ya jopo la maridhiano (BBI) itakapotolewa wiki hii.

Wengine walishangaa kama hali hiyo ilikusudiwa, kwani wakati Rais Kenyatta na naibu wake William Ruto walipoingia mamlakani walikuwa na tabia ya kuvaa mavazi ya kufanana mara kwa mara kuonyesha ushirikiano wao.

Wakati wa sherehe za Jumapili, usalama katika kivuko cha Likoni uliimarishwa huku Jeshi la Wanamaji likichukua usukani katika kivuko hicho ambacho kipo karibu na bustani ya Mama Ngina ambapo sherehe ziliandaliwa.

Mamia ya wafanyabiashara wanaohudumu eneo hilo pia waliondolewa.

Mamia ya wakazi kutoka maeneo tofauti ya Pwani walikusanyika kuanzia saa kumi na moja alfajiri kwa sherehe.

Ilibidi baadhi ya waliofika kuzuiwa wasiingie huku wengine wakipanda juu ya miti ili kufuatilia yaliyokuwa yakijiri.

Ukarabati

Katika hatua moja ilibidi maafisa wa usalama kutumia nguvu kutuliza umati na watu kadhaa wakaondolewa katika bustani hiyo ili kurudisha hali ya utulivu.

Wengi waliofika katika eneo hilo walisema walitaka kushuhudia ukarabati ambao umefanyiwa bustani ya Mama Ngina kwa gharama ya Sh400 milioni.

Ilikuwa mara ya kwanza Jeshi la Wanamaji kuandaa sherehe hiyo, na kufanya maonyesho yaliyofana baharini.

Maonyesho yao yalijumuisha msafara wa maboti ya kijeshi na meli ambazo ndizo zilitumiwa kufyatua makombora ya heshima.

Kikosi cha jeshi la wanahewa pia kilifanya maonyesho yake angani kwa madoido yaliyojumuisha rubani wa helikopta kuisimama hewani.

 

Imeripotiwa na Mishi Gongo, Ahmed Mohamed na Valentine Obara