Habari Mseto

Mavuno ni tele lakini hakuna walaji Nyandarua

November 18th, 2020 1 min read

Na WAIKWA MAINA

WAKULIMA wa Kaunti ya Nyandarua wanavuna mavuno yaliyoongezeka maradufu lakini hawana hela mifukoni.

Katika eneo lenye ukame la Ndaragua, wakulima wa mahindi wamevuna misimu mitatu huku wengine wakitazamiwa kuvuna msimu wa tatu kufikia Januari.

Bi Rosemary Wanjiru, mkimbizi wa Ndani kwa Ndani (IDP) aliyepata makao Ndaragua alikuwa na vipindi viwili vya mavuno mwaka huu huku akiwa na mazao ya mahindi yanayosubiri kuvunwa kati ya Januari na Februari.

Katika eneo la Kinangop ambalo limegubikwa na baridi katika miaka kadhaa iliyopita, wakulima wa mboga walikuwa na mavuno tele kutokana na mvua ya kutosha.

“Mazao ya kabeji ambayo kwa kawaida huwa tayari kuvunwa Januari yako tayari kuvunwa. Hali ya anga ilikuwa shwari bila barafu nyingi, hali iliyofanya mboga kukua haraka kwa gharama ya chini ya uzalishaji inayotokana na hali ya anga yenye baridi kupindukia,” alisema Bi Millicent Gathoni.

Lakini licha ya mavuno hayo tele, wakulima hao wanalalamikia ukosefu wa soko, hali ambayo walihusisha na kukomaa mapema na mavuno tele ya mazao. Katika maeneo ya Kinangop, Kipipiri, na Ol Kalou, kabichi zinaozea shambani kutokana na ukosefu wa soko.

Mawakala wachache wanaotembelea mashamba hayo wanatoa Sh20 kwa kabichi saba. Mboga hizo sasa ni kitoweo cha mifugo ambao pia wamezikinai.

“Niliwekeza Sh70,0000 katika shamba la ekari moja nikitarajia kuuza kila kabichi kwa Sh20. Nina jumla ya mboga 18,500 ambazo zingenipa Sh370,000 kwa bei hiyo. Nimekata tamaa. Ni hasara kubwa,” alisema Bi Teresiah Nyaguthii.

Wakulima hao wa mahindi pia wanalalamikia bei duni, wakiuza mfuko wa kilo 90 kwa Sh1, 500, ikilinganishwa na Sh2, 000 na Sh2, 300 mwaka uliopita.

“Nashindwa kuelewa ni kwa nini wauzaji wanatoa bei ya chini ilhali mazao haya ni bora zaidi,”alisema Bw Kepha Waweru.