Mavuno ya mahindi kupungua – utafiti

Mavuno ya mahindi kupungua – utafiti

Na BARNABAS BII

WAKULIMA wa mahindi na wataalamu wa Kilimo katika eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa, wameeleza wasiwasi wa kupata mazao haba msimu huu kutokana na kuchelewa kwa mvua huku asilimia kubwa ya mimea iliyopandwa wakati wa kiangazi ikinyauka.

Kupungua kwa mvua kumelazimisha baadhi ya wakulima wa mahindi kupunguza eneo wanalopanda mmea huo kutoka hektari 92,500 hadi 77,225 katika kaunti ya Uasin Gishu. Kaunti hiyo ilipokea chini ya milimita 22.5 ya mvua wakati wa msimu wa upanzi mwezi Aprili.

Kaunti zilizoathiriwa ambazo zilipokea chini ya asilimia 3 ya mvua msimu wa upanzi ( Februari – Aprili) ni Trans-Nzoia, Uasin Gishu, Nandi, Elgeyo Marakwet, Pokot Magharibi, Baringo, Nakuru na Bungoma.

Kaunti hizi ndizo zinazotoa mahindi kwa wingi nchini.

Wakulima wa mahindi hupanda mumea huo kati ya Februari na Aprili na kiangazi kinachoshuhudiwa kwa sasa kinahatarisha ukuzaji mahindi.

“Kwa sababu ya uhaba wa mvua wakati wa msimu wa upanzi, ni asilimia 30 ya mbegu zilizomea na hali inaweza kuwa mbaya zaidi mvua ikikosa kunyesha,” alisema Joseph Kosgei, mtaalamu wa Kilimo anayehudumu Eldoret.

Wizara ya Kilimo inabashiri kwamba mavuno ya mahindi yatapungua kwa asilimia 20 ya magunia 40 milioni yaliyotarajiwa kuvunwa.

Uhaba wa mvua msimu wa upanzi na uvamizi wa viwavijeshi umelaumiwa kwa kupungua kwa mavuno ya mahindi.

Shirika la Agricultural Information Network (GAIN), la wizara ya kilimo ya Amerika linabashiri kwamba mavuno ya mahindi, ngano na mchele yatapungua msimu huu kutokana na kupungua kwa eneo ambalo mazao hayo yanakuzwa dhidi ya ongezeko la mahitaji ya nafaka hizo zinazotumiwa na watu wengi kwa chakula.

“Mavuno ya mahindi yanabashiriwa kupungua kwa tani 3.6 milioni 2019-20 kutoka 4.05 milioni mwaka wa 2018-19,” inaonya ripoti ya Amerika.

Hali hii ya kupungua kwa mavuno pamoja na wakulima kukosa motisha kunakotokana na bei duni ya mahindi sokoni msimu uliopita.

Kaunti ya Uasin Gishu ilizalisha magunia 4.5 milioni ya mahindi msimu uliopita lakini yanatarajiwa kupungua msimu huu mmea huo unaponyauka kwa sababu ya kiangazi.

“Kiangazi kinachoendelea ni pigo kwa wakulima ambao watapata hasara zaidi iliyosababishwa na kupanda kwa bei za mbolea na mafuta,” alisema Jackson Kosgei kutoka Moiben kaunti ya Uasin Gishu.

Katika kaunti ya Trans-Nzoia, mavuno ya mahindi yanatarajiwa kuwa magunia 4.7 milioni kutoka 5 milioni msimu uliopita huku baadhi ya wakulima wa mahindi wakigeukia kilimo cha miwa.

Waziri wa kilimo wa kaunti hiyo Mary Nzomo alisema miwa imepandwa katika ekari zipatazo 5000 na nyingine 2000 zinatayarishwa kupandwa mumea huo hatua ambayo inatia wasiwasi.

You can share this post!

Majaji wakemea Uhuru, wamzuia kujadili kesi, BBI

Duale aitaka serikali ya Korane iimarishe huduma Garissa