MAWAIDHA YA KIISLAMU: Baadhi ya njia ambazo Mu’umin atatumia kuimarisha imani yake

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Baadhi ya njia ambazo Mu’umin atatumia kuimarisha imani yake

Na HAWA ALI

KILA sifa njema zinamstahikia Allah Mola wa viumbe vyote.

Sala na salamu zimuendee Mtume wetu Muhammad (swalla Allahu alaihi wa sallam) na ahli zake na maswahaba wake.

Imani ya mja huwa inapanda na kushuka. Na hii ni miongoni mwa tabia za muislamu. Kuna wakati muislamu imani yake humjaa na huwa anajitahidi katika Ibada.

Sala tano hazimpiti tena kwa jamaa. Funga za sunna huwa ndio vazi lake. Adhkaar na sala za usiku ndio mapambo yake. Lakini baada ya muda haya mambo yote huwa hayafanyi tena. Na huanza uvivu wa kutekeleza mambo hayo.

Wengine wao huwa na imani kubwa sana na hamu ya kutenda matendo mema na nia hasa pale wanapokumbushwa.

Ila baada ya muda hamu ile ya kufanya ibada inapotea. Lakini hawa wote tujiulize ni kipi kinachowafanya wawe hivyo?

Tatizo lao ni udhaifu wa imani au kushuka kwa imani. Imani inapokuwa juu basi ndipo kheri zote huzikimbilia au ndipo hamu ya kufanya ibada humjaa mtu. Lakini imani inaposhuka basi huyu mtu huwa hana tena hamu ya mambo hayo na huwa na uvivu. Sasa nini afanye ili aipe nguvu imani yake? Leo katika makala hii tutajaribu kuelezea baadhi ya njia ambazo Muislamu anaweza kuzifanya ili aweze kuipa nguvu imani yake. Njia zenyewe ni kama zifuatazo:

1-Kuomba dua kwa Allah akujaalie imani thabiti

Hakika kila jambo ikiwa unamuomba Allah (subhanahu wataala) basi Allah atakupatia jambo hilo. Hivyo basi jambo muhimu muombe dua Allah (subhanahu wataala).

2-Kusoma Quraan kwa mazingatio

Endapo muislamu anapohisi imani yake imeshuka au inatetereka basi akimbilie kusoma sana Quraan. Ila aisome Qur’an kwa mazingatio kwa kujua ni kipi ambacho Allah (subhanahu wataala) anakielezea ndani ya Qur’an. Na ikiwa mtu hajui tafsiri ya Qur’an basi asome kwa kutumia msahafu wa tafsiri.

Hakuna yeyote ambae amesoma Quraan kwa mazingatio isipokuwa umelainika moyo wake. Na hapo ndipo sifa ya muumini inapopatikana. Na endapo ukaona kuwa unasoma Quraan na moyo wako hauathiriki na chochote basi jua wewe ni maiti inayotembea duniani.

3- Kukithirisha kukumbuka mauti

Mauti ni safari ya lazima kwa kila mwanadamu. Nayo ni safari ya kutoka katika dunia katika maisha ya mpito na kuelekea katika maisha ya akhera. Mwanadamu yanapomkuta mauti basi muda wa mtihani wake ndio unakuwa umekwisha na kinachobaki ni kwenda kukutana na hesabu.

Je ulishwahi kujiuliza ni vipi roho yako itatolewa?

Itatolewa kwa ajili ya kwenda jannah au itatolewa kwa ajili ya kwenda motoni?

Je ulishawahi kujiuliza vipi itakuwa hali yako pale utakapokuwa umebebwa kwenye jeneza?

Je ulishawahi kukaa na kujiuliza vipi utaikuta hesabu yako?

Je umeshawahi kujiuliza nini utamjibu Allah pale utakaposimamishwa mbele yake?

Mauti ni mazingatio tosha kwa muislamu na kumkumbusha ili aweze kukaa katika njia ya Allah (subhanahu wataala).

4-Kutembelea makaburi

Makaburi nayo yana siri nzito ndani yake. Tayari tumeshamuhifadhi ndugu yetu katika kuelekea katika maisha yake ya milele. Nini kinachojiri ndani ya mauti.

Mwanadamu atakapokaa na kuliwaza kaburi, giza lake na juu yake kufukiwa na michanga. Vipi atakaa ndani ya shimo hilo? Je ulishawahi kujiuliza vipi itakuwa usiku wa kwanza ndani ya kaburi lako?

Je wakati watu watakapokuwa washamzika ataweza kujibu maswali ya Munkar na Nakir? Je kaburi lake litakuwa ni bustani katika bustani ya peponi au mashimo katika mashimo ya motoni?

Tembelea makaburi ili uizidshe imani na uwe ni mwenye kujiandaa daima na kukaa katika kaburi lako.

5-Kusoma historia za wema waliopita

Kusoma historia za wema waliopita na vipi walivyokuwa wakijituma katika ibada na kutafuta radhi za Allah ni moja kati ya njia ya kumfanya mja daima awe na hamu ya kuwa katika utiifu.

Maana atakuwa anaona hali halisi ya vipi watu waliisamehe dunia na kuipenda akhera. Wakatosheka na dunia,wakatarajia ya akhera. Kama tulivyotoa mfano vipi kina Sayyidina Umar walivyokuwa wakiisoma Quraan.

6- Kukaa na marafiki wema na kushiriki vikao vya kheri

Rafiki huchangia kwa kiwango kikubwa maisha ya binaadamu. Na hili linathibitishwa na Mtume Muhammad (swalla Allahu alayhi wasallam) kwa kauli yake pale aliposema “Mtu hufuata mwenendo wa rafiki yake,basi aangalie mmoja wenu ni nani anaemfanya kuwa ni rafiki” Attirmidhy.

Jitahidi sana na kuwaepuka marafiki waovu kwani hawawezi kukusaidia katika kuikuza imani yako. Kaa na rafiki mwema rafiki ambae daima atakuwa ni mwenye kukuhimiza katika kufanya yalo mema na yaliyo mazuri. Tumeona mifano ya wengi ambao wamepotoka kwa sababu tu ya marafiki.

You can share this post!

KINYUA BIN KING’ORI: Vita dhidi ya jinamizi la...

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Mola Subuhaanahu Wata’ala ndiye...