MAWAIDHA YA KIISLAMU: Dunia ya leo yahitaji dua kwa wingi kutokana na shida tele

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Dunia ya leo yahitaji dua kwa wingi kutokana na shida tele

NA ALI HASSAN

ASSALLAM Aleykum ndugu yangu muumin wa dini hii tukufu ya Kiislamu.

Kwa jina lake Mwenyezi Mungu mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na neema ndogo ndogo, tumejaaliwa leo kukutana katika ukumbi wetu huu mtukufu wa kuambizana mawili matatu kuihusu dini yetu ya Kiislamu.

Awali ya yote, tuchukue uzito wa nafasi hii kumshukuru, kumhimidi, kumtukuza na kumpwekesha Muumba wetu, Allah (SWT). Ni yeye pekee ndiye anayestahili kuabudiwa. Ni yeye pekee ndiye Muumba wa ardhi na mbingu. Ni yeye pekee ndiye kaumba viumbe vyote.

Hakuna mwingine anayestahili kuabudiwa ile ni yeye pekee: Mwenyezi Mungu.

Ama baada ya kumpwekesha Muumba wetu, twachukua sawia nafasi hii kumtilia dua na kumfanyia kila aina ya maombi mwombezi wetu, Mtume (SAW). Na papo hapo pia nasi waumini wa dini hii tukufu ya Kiislamu inatupasa kujitahidi kufanya mema, kuepukana na mawi na kujizika zaidi katika mafunzo ya dini, na sunna za Mtume (SAW).

Leo hii ndugu yangu tunazungumza kwenye makiwanda haya ya mawaidha tukiwa kwenye maruerue ya baada ya uchaguzi mkuu nchini. Na tukio hilo la uchaguzi limezua matukio mbali mbali mbali ambayo yatantufanya sisi waja-waumini kuzidisha ibda, kumshukuru Mola na kujitahidi kufanya ibada kila kukicha.

Sasa hivi kuna lawama za hapa na pale kuhusu kupanda kwa gharama ya maisha. Kikubwa kikitokana na ongezeko la bei za mafuta. Hali hii imefanya uchumi kuzidi kudoda. Serikali iliongia mamlakani ikidai kuwa serikali imecharara. Kwa maana hiyo ni kuwa kila mmoja anadaiwa kope si zake!

Uchumi wa nchi umezorota mno! Hakuna tena utoshelevu wa chakula. Matokeo yake ni visa vya kihuni kama vile kudorora kwa hali ya usalama, visa vya mauaji, kukata tamaa, na kila aina ya unyama.Subhannallah!Leo hii ndugu yangu inabidi tukumbukane kwenye maombi. Kaunti kadha nchini zimetabiri ukame.

Mifugo haina malisho. Mimea imekauka na kunyauka! Hali ni ngumu yakhe! Mvua zimetugomea. Tunahitaji dua na maombi maalum ili pawepo na mvua.

Ubadhirifu nao unazidi kufanyika katika jamii zetu. Watu, wezi, wanaiba mali ya umma. Maisha yanazidi kuwa magumu. Ewe Mola wetu tuonee Imani.

Hivi tunavyozungumza, bei za nguvu za umeme zimepanda na kupanda! Bei za kawi, gesi, vyakula, yaani kila bidhaa, zimekuwa zikipanda na kupaa hadi angani, sikwambii nauli. Uchukuzi umetatizika mno.

Dunia nzima haijapona kutokana na janga la virusi vya Corona. Halafu, tukingalia kuathirika na kukwazika kutokana na athari za virusi vya Corona, nayo mapigano ndio hayo. Binadamu hawapendani ati!

Unazungumziaje vita vikali, mauaji ya kila nukta, na uhasama wa silaha unaoshuhudiwa katika nchi mbali mbali duniani. Sio Sudan Kusini, sio Somali, sio Uhabeshi na kwingi kwingineko. Hali ya maisha imezidi kudorora zaidi kufuatia mapigano makali ambayo yanaendelea baina ya Ukraine na Urusi.

Vita hivi vimeathiri nchi husika, nchi jirani, na dunia kwa ujumla. Unga haumudiki kabisa. Fatalaiza usiseme mwenzangu. Mahindi yamekuwa ghali kama dhahabu.Ulimwengu nao kimyaa!Sio runinga, sio magazeti, sio maredio, kila kukicha mchafuko unazidi kutokota.

Mauaji ni kama mchezo wa kitoto. Ukraine si nchi tena. Ni vigae tu. Ni mahame tu. Ni magofu tu yakhe. Hadi lini jamani? Mbona binadamu tumeruhusu kuingiwa na unyama na kutawaliwa na umero, ufisadi, ubabe na unyama wenye ukatili hata kuliko unyama katika mbuga ya wanyama.

Sasa hivi lipo tishio la mkurupuko wa maradhi ya Ebola. Tumeshuhudia cha hivi punde zaidi katika nchi jirani ya Uganda.

Taharuki hii inatufunza nini ndugu yangu? Hakuna jambo linafanyika ila kwa mapenzi yake Maulana.Dunia ya leo imejawa na maovu. Dunia ya sasa imepungukiwa na wema. Kizazi cha sasa kimejawa na ukatili na udhalimu. Kwa maana hiyo ni kuwa tunahitaji mno maombi. Dua kwa wingi. Cha kushangaza ni kuwa waja wamejisahau. Tunajibidisha mno kusaka maisha. Tupo mbioni kuzitafuta hela. Tunasahau kuwa Mungu yupo.

Hatumkumbuki Mola wakati mambo yanatunyookea. Kukitokea nuksi, mkasa, janga ndio tunaanza kumlilia Maulana.Ndugu zangu, tuzidishe ibada. Tuzidishe maombi. Ndio silaha pekee tulio nayo sisi waja. In Shaa Allah iwe siku ya maombi.

Ijumaa Kareem!

alikauleni@gmail.com

  • Tags

You can share this post!

Macho kwa Neymar timu ya Brazil ikiendea Ghana kirafiki leo

Mashirika yataka adhabu kali kwa wauaji wa wazee

T L