Makala

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Hatari ya kuihama Qur’an Tukufu

April 26th, 2019 2 min read

Na HAWA ALI

SIFA zote njema anastahiki Mola Azzawajalla, Mwenye kuneemesha neema kubwakubwa na nyingine ndogondogo.

Swala na salamu zimwendee Mtume wetu Muhammad, rahmatan lil ‘alamiyn, maswahaba wake kiram na watangu wema hadi siku ya Kiyaamah.

Allah Azzawajalla Anatuambia jinsi Mtume SAW Alivyokuwa akilalamika kuwa watu wake wameihama na kuipuuza hii Qur’an.

Makafiri Quraysh walikuwa hawataki kusikiliza Qur’an, na ilipokuwa ikisomwa walikuwa wakizungumza upuuzi au kuzungumza kwa sauti za juu mazungumzo mengine ili wasiisikie.

Hali hii ya kuipuuza Qur’an vile vile iko miongoni mwa Waislamu hali kadhalika, ingawa Waislamu tofauti yake ni kuwa wameiamini na sio kama Makafiri Quraysh ambao ilikuwa ni dhaahiri kuwa waliikanusha na kutoiamini.

Wafasiri Wa Qur-aan wameifafanua Ayah hiyo ya kwanza inayosema, ((Hakika watu wangu wameifanya hii Qur-aan ni kitu kilichohamwa (kilichoachiliwa mbali)) kwamba: kuihama na kupuuza Qur-aan inawahusu watu wa aina zifuatazo:

Wasioisoma kabisa.

Wanaoisoma lakini hawajifunzi maana yake.

Wanaoisoma na kujifunza maana yake lakini hawafuati maamrisho yake na hawajiepushi na makatazo yake.

Kuihama Qur’an na kuipuuza ni hatari kubwa kabisa na Mola wetu Mtukufu Ametuonya na Kututisha kupitia Aayah nyingi za Qur’an.

Miongoni mwa maonyo hayo ni kwamba mja atakuwa na maisha ya dhiki na hufufuliwa siku ya Qiyaamah akiwa kipofu kama ifuatavyo:

Na atakayejiepusha na mawaidha Yangu, basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki, na Siku ya Qiyaamah Tutamfufua hali ya kuwa kipofu ((Aseme:

Ee Mola wangu, mbona Umenifufua kipofu, nami nilikuwa nikiona?)) Allaaha Azzawajalla Atasema: Ndivyo vivyo hivyo. Zilikufikia ishara Zetu, nawe ukazisahau, na kadhaalika leo unasahauliwa)) [Twaaha: 124-126]

Ndugu Waislamu tunaona hatari ya kuipuuza Qur’an na kuihama basi na tujitahidi kuisoma, kujifunza maana yake na kufuata maamrisho yake na kujiepusha na makatazo yake ili tuwe miongoni mwa wale Aliowasifu Allah Subuhaanahu Wata’ala katika hii Qur’an kuwa wanaisoma ‘ipasavyo.’

Zifuatazo ni kauli za Maswahaba Ridhwanullah A’alayhim ajmai’in kuhusu ‘kuisoma ipasavyo’

Ibn Mas’uud RA “Naapa kwa Yule Nafsi yangu iko mikononi Mwake, Tilaawa ya kweli ni kufuata yaliohalalishwa na kuacha yaliokatazwa, kusoma kama ilivyoteremshwa, kutokubadilisha maneno katika sehemu zake na kutokuifasiri vingine na ilivyopasa kutafsiriwa” [At-Twabariy 2.567]
Ibn ‘Abbas RA Wenye kuhalalisha yaliyo halali na kukataza yalioharimishwa na hawabadilishi maneno yake”. [At-Twabariy 2.567]
‘Umar bin Al-Khattwaab RA: “Ni wale ambao inaposomwa Aayah na inapotajwa Rehma wanamuomba Allaah Azzawajalla Rehma Yake, na wanaposoma Aayah inayotaja adhabu, wanajikinga kwa Allaah Subuhaanahu Wata’ala nayo”. [Al-Qurtubiy 2:95]