Habari Mseto

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Hayawani sasa nafuu, binadamu wamevuka mipaka!

January 19th, 2024 2 min read

Na ALI HASSAN

KWA jina la Mwenyezi Mungu mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na neema ndogo ndogo. Tumejaaliwa siku hii aula, tukufu na bora ili kuambizana, kuhimizana na kusemezana kuihusu dini yetu tukufu ya Kiislamu.

Awali ya yote tumshukuru, kumhimidi na kumpwekesha Mola wetu mmoja, Allah (SWT). Ni yeye pekee ndiye Muumba wa ardhi na mbingu na vyote vilivyomo. Ama katika usanjari huo wa kumsifu, kumshukuru na kumpwekesha Mola wetu, tunamshukuru pia kwa kutujaalia sisi kuwa waumini wa dini hii tukufu ya Kiislamu.

Ama ndugu yangu leo hii gumzo letu linahusu mauaji. Ulimwengu umejaa na kutapakaa mauaji. Binadamu wanauana kama kuku. Waja tunachinjana kama wanyama wa mbugani. Mauaji ya kikatili ambayo hata wanyama, mahayawani hasa, wanaonea aibu.
Subhannallah

Ya Rabi Mola wetu

Kulikoni? Binadamua ndio kama sasa hivi ameingiwa na kichaa cha mauaji. Mitandao, vyombo vya habari vimejaa picha za kuogofya mno!

Wanandoa wanachinjana kinyama. Visa ni tele! Binadamu ni kama tumekata tamaa. Ugumu wa maisha ati? Kila nukta, saa na sekunde, watu wanajitia vitanzi. Picha na video zimetamalaki mitandaoni. Watu wanajirusha na kujiua kutoka kwenye maghorofa.
Vyumba vya kukodi vya watu kulala ndio usiseme! Kila kukicha afadhali ya jana!

Maafisa wa polisi wanapata taabu kuibeba miili na kuchunguza visa vya mauaji. Ndugu zetu hawa wanahitaji mafunzo ya kisaikolojia. Miili ya mabinti zetu, hadi vyuoni, inapatikana imefanyiwa unyama kuliko unyama. Kubakwa!

Na kisha kuchinjwa! Mingine imechanwa-chanwa na kuchanjwa. Inakuwa chinyango hasa! Ni itikadi gani hizi yakhe! Au ni biashara gani hii ya viungo vya miili ya watu?

Dunia imepasuka wapi? Angeuliza mwanahabari P.P Mwai, marehemu sasa, zama zake kwenye kipindi cha Yaliyomo.

Nchi zinatenga mabilioni kwa mabilioni ya hela katika bajeti kununua silaha ili ama kushambulia au kujihami. Viongozi wenye rasilmali na uwezo mkubwa wa uchumi, wamefumba vinywa na macho yao.

Wanasema: “LANGU JICHO”! Ilhali dunia inachomeka, kuungua na kuteketea.

Huko Gaza, takriban miezi mitatu sasa, binadamu wanauana tu. Siwambii Urusi na Ukraine! Vipi Sudan? Jamhuri ya Demokrasi ya Kongo je?

Ewe Mola wetu tunusuru. Tunakulilia. Ya Rabi.

Ijumaa Mubarak

[email protected]