Makala

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Ibada za usiku zina ujira mkubwa hasa katika mwezi huu wa Ramadhani

May 24th, 2019 3 min read

Na ALI HASSAN

KWA jina la Mwenyezi Mungu mwenye kuneemesha neema kubwakubwa na neema ndogondogo.

Ni siku nyingine tukufu tunapokutana ili kuadhiana kuihusu dini yetu tukufu ya Kiislamu.

Mawaidha ya leo yakikolezwa zaidi na utamu wa kutujieni tukiwa katika funga ya lazima, funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Kama ilivyo ada na desturi ya dini yetu tukufu ya Kiislamu, twatanguliza kila jambo, kila kauli, kila shughuli kwa kumshukuru mno Muumba wetu kwa kutuneemeshia neema ya uhai ili kuzidisha ibada.

Kwa maana hiyo sharuti kumshukuru Muumba wetu na kuzidisha ibada.

Kadhalika, katika uzi uo huo wa ufunguzi, twamtilia dua na kutakia mema bwana wetu, Mtume (SAW).

Leo hii ndugu yangu muumin tumekutana huku tukizidi kuufurahikia utamu wa saumu. Mbali na ibada mbali mbali saa ishirini na nne za mfungo huu, kikubwa ni kuhusu ibada muhimu nyakati za usiku kwenye mwezi huu.

Hilo lamaanisha kuwa usiku wa Ramadhan sio wakati wa kula, kunywa na kuvimbiwa.

Vilevile, usiku huu wa Ramadhani si wakati wa kujikita katika mambo ya kihuni kama kuvuta sigareti, kula gomba, kucheza michezo ya dhumna, drafu na kadi.

Bali ni usiku wa ibada chungu nzima, achia mbali kutubia na kuisoma Kurani.

Imepokelewa kutoka kwa Bi Aisha akisema: “Alitoka, Mtume (SAW) usiku mmoja akaenda kuswali msikitini. Watu wakamfuata nyuma katika Swala yake hiyo. Kulipokucha, watu wakawa wanaambizana kuhusu swala hiyo. Hivyo, watu wengi zaidi wakajumuika, siku ya pili. Mtume akaenda tena usiku wa pili, msikitini. Watu wengi zaidi wakamfuata katika swala yake hiyo. Kulipokucha, watu wakaanza kuambizana kuhusu swala hiyo. Hivyo, watu wakajumuika, kwa wingi zaidi msikitini.

Mtume akaenda tena usiku wa siku ya tatu, ambako kulikuwa na watu wengi zaidi. Akaswali siku ya tatu, na watu wakamfuata kwa swala yake hiyo.

Ilipoingia alfajiri ndiyo akaenda msikitini kwa swala ya alfajiri.

Alipomaliza kuswali alfajiri, aliwageukia watu na kutoa Shahada, na kisha kusema:

“Amma Ba’d! Si kama nilikuwa sijui kuhusu kujumuika kwenu, jana usiku, msikitini! Nilikuwa najua vilivyo! Ila nilichelea isije swala hiyo ikafaradhishwa juu yenu, na halafu mkashindwa kuitekeleza.” Muttafaq Alayhi.

Abu Hurayra akisema: Amesema Mtume (SAW):

“Atayefanya ibada usiku wa mwezi (mzima) wa Ramadhani, kwa imani safi kabisa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, huku akiwa na matarajio ya malipo ya Mwenyezi Mungu, Pekee, atafutiwa madhambi yake yote yaliyotangulia.”

Imepolekewa, vilevile, kutoka kwa Abu Hurayra akisema: “Alikuwa Mtume (SAW) akiwahimiza sana watu kufanya ibada usiku wa mwezi wa Ramadhani (mzima) pasi na kuwalazimisha, kwa kusema:

“Atayefanya ibada usiku wa mwezi (mzima) wa Ramadhani, kwa Imani safi kabisa kwa Mwenyezi Mungu, huku akiwa na matarajio ya malipo ya Mwenyezi Mungu, Pekee, atafutiwa madhambi yake yote yaliyotangulia.” Ameipokea Muslim.

Swala ya Tarawehe ni sunna maarufu, inayoswaliwa baada ya swala ya Isha, kila siku, usiku, katika mfungo wa Ramadhani. Na imeitwa Tarawehe, kwa sababu baada ya kila rakaa nne, watu hupumzika, kidogo, kisha kuendelea.

Ni swala inayo swaliwa rakaa mbili mbili, kwa kupumzika kidogo, na baada ya kukamilisha rakaaa nne, basi hupumzika kwa muda zaidi.

Ni swala ambayo, sio tu, ameiswali Mtume (SAW) mwenyewe msikitini, bali ameiswalisha jamaa, kwa muda wa siku tatu mfululizo.

Na watu walikuwa wakiongezeka kuja kuswali nyuma yake, kiasi kwamba siku ya nne, msikiti haukutosha! Mtume hakutoka tena kwenda kuswali Swala hiyo, licha ya watu kunadi kuwa wakati wa swala hiyo umewadia. Mtume (SAW) hakuitikia wito wao huo.

Kuswali jamaa moja, nyuma ya Imamu mmoja ni Sunna kutoka kwa Mtume (SAW) na vilevile, ni sunna aliyeiendeleza, rasmi, Sayyidina Umar nyuma ya Sayyidina Umab bin Ka’b!

Mwenye kusimama kufanya Ibada Usiku wa Ramadhani, kwa nia safi, na kutaraji Fadhila za Mwenyezi Mungu, tu, hufutiwa madhambi yake yaliyopita.

In Shaa Allah ndugu zangu waumini wa dini hii tukufu ya Kiislamu tujikaze kusali swala ya tarawehi.

Ijumaa Kareem!

[email protected]