Makala

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Jiandae na maisha ya barzakh ambayo hayana salama ila kwa wacha-Mungu

November 29th, 2019 4 min read

Na HAWA ALI

SIFA zote njema anastahiki Mola Azzawajalla, Mwenye kuneemesha neema kubwakubwa na nyingine ndogondogo.

Swala na salamu zimwendee Mtume wetu Muhammad, rahmatan lil ‘alamiyn, maswahaba wake kiram na watangu wema hadi siku ya Kiyaamah.

Nini kufa? Kufa ni kuepukana roho na kiwiliwili, au kufa ni kukatika matumizi ya roho kwa kiwiliwili na kukosa kiwiliwili ala yake na kumuepusha mtu na amali yake na watoto wake na mke wake.

Kufa kunakata utamu wa maisha ya kilimwengu na kwenda ulimwengu mwengine. Mtu ambaye alikuwa akifurahia maisha ya ulimwengu amepata khasara baada ya kufa.

Na yule ambaye alikuwa akifurahi kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu basi atapata neema kubwa na inakamilika kufaulu kwake.

Watu wengi hudhania ya kwamba mtu anapokufa na akazikwa amemaliza kila kitu na amepumzika na ulimwengu, wala halimjii yeye jambo lolote.

Kudhani hivyo ni kosa kubwa bali hakika mwanadamu baada ya kufa kwake anaingia katika maisha mapya, maisha ya barzakh na kutoka maisha ya barzakh huenda kwenye maisha ya akhera ambayo ndiyo maisha ya mwisho na ya milele.

Hakika Qu’ran imebainisha wazi na Hadithi za Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) yatakayotokea baada ya kufa. Wakati anapokufa Mwanadamu na akazikwa, jambo la kwanza linalompata ni fitina ya kaburi.

Imepokewa katika sahihi mbili ya Bukhari na Muslim kutoka kwa Anas Bin Malik Akipokea kutoka kwa Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): Hakika mja anapowekwa katika kaburi lake na wakaondoka watu wake, Anasikia mlio wa viatu vyao. Akasema wanamjia Malaika wawili wakamkalisha wakamuambia unasemaje juu ya mtu huyu. Akasema: Ama Muislamu atasema: Nilikuwa nikishuhudia ya kwamba ni mja wa Mwenyezi Mungu na ni Mtume wake. Akasema: Ataambiwa angalia makao yako motoni umebadilishiwa pepo. Akasema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) Atayaona makao mawili. Amesema Qatada tumeelezwa: hukunjuliwa kaburi lake dhiraa sabini na atajaziwa kila aina ya chakula. Ama aliye kufuru na mnafiki ataulizwa unajua nini juu ya mtu huyu atasema sijui nilikuwa nikisema walivyokuwa wakisema watu ataambiwa hukujuwa na wala hukusoma atapigwa nyundo ya chuma moja moja, watasikia watu wote wasiokuwa viumbe aina mbili (wanadamu na majini)].

Na imepokewa na Abu Ayyub radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie Amesema : Alitoka Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) na jua limetoka, Akasikia sauti ya Yahudi anaadhibiwa katika kaburi lake’ (Bukhari na Muslim). Kwa hivyo, Alikuwa Mtume haswali swala yeyote ila alikuwa akijilinda na adhabu ya kaburi. Na akaamrisha hivyo watu wake].

Kisha ataadhibiwa kafiri na mnafiki. Na Mu’mini atastarehe. Basi tujiulize nafsi zetu, je tumeandaa jawabu ya masuali ya kaburini. Ewe mja wa Mwenyezi Mungu, hakika hiko ni kiyama kitakuja hakina shaka. Na baada yayote atawafufuwa Mwenyezi Mungu walioko kwenye makaburi. Na dalili ni Aya tukufu:

{{Je hatambui mwanadamu ya kwamba tumemuumba kwa tone la manii? Mara amekuwa hasimu Yetu aliye dhahiri. Na akatupigia sisi mfano, na akasahau kuumbwa kwake. Akasema ni nani atakayeihuisha mifupa na hali imesagika?. Sema Ewe Muhammad; Ataihuisha Yule aliyeiumba mara ya kwanza na yeye ni mjuzi wa kila namna ya kuumba}} [Yaasin : 77 – 79]. Halafu atawakusanya watu wote kwa ajili ya hisabu. Amesema Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala):

{{Na tuwakusanya siku ya kiama hali kuwa wanakokotwa juu ya nyuso zao na hali ya kuwa ni mapofu na mabubu na viziwi. Makazo yao ni Jahannamu. Kila ukifanya kusinzia kidogo tutawazidishia mwako}} [Israai : 97].

Haya ndiyo matukio ya kuogopesha utawaona wabaya na madhalimu na wana fiki wameinamisha vichwa vyao, hawarudishi macho yao, wala hasemi siku hiyo ila aliye pewa ruhusa na Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala). Na nyoyo siku hiyo zimefika kooni wamekasirika na madhalimu hawana muombezi wala rafiki mwenye kutiiwa. Na siku hii kiasi chake ni miaka khamsini alfu.

Waja wa Mwenyezi Mungu, wakati huo watu watasimama mbele ya Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala), hakuna pa kufichika. Siku hiyo watu watatoka makaburini vikundi vikundi kwa ajili ya kuona vitendo vyao. Na itaanza hisabu. Amesema Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): [ Ataletwa kafiri siku ya kiama aambiwe waonaje lau ungekuwa na mjazo wa ardhi dhahabu ungalijikomboa? atasema ndiyo. Ataambiwa umeulizwa ambalo ni sahali kuliko hilo]. Na katika mapokezi mengine: [Nimekuuliza ambalo ni sahali kuliko hili na wewe uko katika mgongo wa Adam usimshirikishe Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) ukakataa na ukanishirikisha na viumbe vingine].

Enyi waisilamu haya ni baadhi ya yale yatakayo tokea siku ya kiama, mbali na yale tuliyo ghafilika nayo. Na kila mmoja katika sisi atakuwa juu ya yale aliyo yafanya katika maasi. Ewe hakimu, Ewe Rais, utatubia lini? Rudi kwa Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala). Utamwambia nini Mola wako. Je hukumbuki neno la Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam): Hakuna mchungaji yeyote aliyepewa uchungaji na Mwenyezi Mungu, atakufa siku atakayokufa na yeye ni mdanganyifu ila ataingia motoni.

Enyi mawaziri na manaibu hamuogopi Mwenyezi Mungu kwa mliyoyabeba juu ya mabega yenu. Je mume jiandaa vipi na hali hii ya utisho miongoni mwa fitina ya kaburi na adhabu yake kukusanywa kwa ajili ya hisabu. Nini mumejiandaa na siku hiyo. Ewe Mwenye kufanya khiyana, Je utawacha lini khiyana zako, utasimamisha lini swala. Rudi kwa Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala). Na wewe mwizi utaaacha lini wizi wako kwa hakika huna budi lazima upitie njia hii ngumu. Na wewe barobaro umejiandaa vipi na siku hii. Je umejiandaa na siku ya kufa. Na wewe msichana wadhani ya kwamba kifo hakitakuja kwako?

Na baada ya hapo zifunguliwe vitabu. Na wenye kupewa vitabu ni aina mbili; ni mwenye kupokea kitabu kwa mkono wa kulia, na mwenye kupewa kitabu kwa mkono wa kushoto. Kisha iwekwe mizani kwa uadilifu siku ya kiama. Baada ya hayo itakuja sirat na kila mmoja atapitia njiya hiyo. Tunamuomba Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) atuafikie tuweze kufaulu katika siku hii nzito.