MAWAIDHA YA KIISLAMU: Maulana atujaalie tuwe na uchaguzi wa kheri

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Maulana atujaalie tuwe na uchaguzi wa kheri

NA ALI HASSAN

KWA jina la Mwenyezi Mungu mwenye kuneemsha neema kubwa kubwa na neema ndogondogo.

Tumejaaliwa leo hii, siku hii tukufu ya Ijumaa, ili kuambizana, kuhimizana na kusemezana kuihusu dini yetu tukufu ya Kiislamu.

Awali ya yote tuchukue uzito wa nafasi hii kumshukuru mwisho wa shukrani Muumba wetu, Mwenye-Enzi-Maulana.

Hakuna mwingine anayestahili kuabudiwa, kuenziwa, kushukuriwa ela Muumba wetu mmoja pekee: Allah (SWT).

Leo hii ndugu yangu nchi yetu iko katika njia-panda!

Ugumu wa maisha, kupanda kwa gharama ya bei za bidhaa, kama sio janga la ukame ni janga la njaa, kama sio ajali za barabarani, ni mikosi na nuksani za hapa na pale.

Allah (SWT) atujaalie iwe kheri. Iwe hatima njema.

Papo hapo kwa hatima nzuri ndipo palipo na uti wa mada yetu leo hii.

Wiki iliyopita kuliandaliwa mdahalo wa urais, ulioshia kuwa kikao cha uliza ujibiwe baada ya baadhi ya wagombeaji wa urais kutofika kwenye mdahalo huo.

Kuandaliwa kwa kikao hicho kukiashiria kukaribia mno kwa uchaguzi mkuu nchini mwetu.

Wakati wa kampeni, ambazo sasa zinaelekea ukingoni, kulishuhudiwa baadhi ya wanadini – na hata viongozi wetu – wakichukua mirengo tofauti tofauti ya siasa.

Hali hii haikuwa picha nzuri kamwe kwa waumini na maamuma.Mfano wa mirengo hii ulionekana kwenye sherehe za kitaifa au hata kwenye dhifa za uzinduzi wa manifesto wa mirengo mbalimbali.

Kwa wale walioalikwa kwenye hafla hizo, walichukuliwa kama ‘wanaomuunga mkono’ aliyewaalika. Na kwa wale walioachwa nje ya mialiko, wakaamua kuchukua misimamo tofauti.

Inasikitikisha kuwa hata baadhi yetu sisi waumini, tunazichukua siasa za nchi na kuzigeuzwa ibada. Dini hasa! Subhannallah!Kabla na baada ya kipindi cha ibada, waumini wanakusanyika katika makundi ya kupiga domo la siasa.

Haina neno. Mushkili uko kwa baadhi yetu sisi kutofautiana kisiasa na kununiana, kufanyiana hiana, na hata kurushiana makonde!

Ya Rabi!Inabidi na kufika kiwango hata hakuna salamu wala kalamu. Au unasikia mwafulani akisema kuwa mimi sitonunua chakula katika hoteli ya mwafulani au sitonunua bidhaa hizi na zile kwenye duka hili na lile kwa kuwa tofauti na hisia kali za siasa zilizomea miongoni mwa nyoyo zetu.

Uchaguzi, tukio la siku moja tu, lakini linaathiri kwa njia mbalimbali maisha yetu. Alikuwa akisema hayati rais Arap Moi kuwa ‘siasa mbaya, maisha mbaya’.

In Shaa Allah tuzidishe ibada. Uwe uchaguzi wa haki, huru na amani.

Ijumaa Mubarak!

alikauleni@gmail.com

  • Tags

You can share this post!

CECIL ODONGO: Madai ya Ruto, Amerika yanalenga kusawiri...

Team Kenya ya Davis Cup tayari kwa Kombe la Afrika tenisi

T L