Makala

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Ndugu yangu, kuchunga muda ni kati ya mambo muhimu kwa muumini

September 13th, 2019 3 min read

Na HAWA ALI

SIFA zote njema anastahiki Mola Azzawajalla, Mwenye kuneemesha neema kubwakubwa na nyingine ndogondogo. Swala na salamu zimwendee Mtume wetu Muhammad, rahmatan lil ‘alamiyn, maswahaba wake kiram na watangu wema hadi siku ya Kiyaamah.

Leo tutagusia umuhimu wa Muislamu kuchunga muda wake na kutokuuangamiza kwa kufanya mambo ya kipuuzi ambayo hayatomsaidia si duniani wala Akhera. Waislamu wengi tunashinda siku kutwa na kujishughulisha na mambo ya kipuuzi ambayo mengi katika yao hayamridhishi Allaah.

Kwanza kabla ya kuendelea tungependa kurudi nyuma kidogo tukumbushane lengo la sisi kuwa hapa duniani ni lipi, kwa nini Mwenyezi Mungu ametuumba. Allah anasema katika Qur-aan:

“Nami sikuwaumba majini na watu ila waniabudu Mimi.”

Hapa tumeona kuwa lengo kubwa la Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) kutuumba ni sisi kumuabudu Yeye, na kama tunavyosimuliwa na Wanachuoni wetu maana ya “Ibaadah” kijumla ni kila Anachokipenda Allah na kukiridhia basi hiyo ni Ibaadah bila shaka.

Moja kwa moja tukirudi katika mada yetu ya kuhusu umuhimu wa kuchunga wakati, tutaona kwamba wengi wetu tumeghafilika na kupuuzia risala hii ambayo ndio lengo kuu la Allah kutuumba. Na tumesahau kwamba kila Muislam hatopiga hatua moja mpaka mbili siku ya Qiyamah mpaka ajibu maswali manne, na moja kati ya hayo ni “Muda wako uliutumia katika mambo gani.”

Ndugu Mwislamu tuzingatie kuwa kila mmoja wetu ataulizwa kwa kila dakika yake moja aliitumia katika mambo ya kheri au ya shari. Utamkuta Muislamu amekaa tu na kulalamika kwamba anahisi uvivu kisa hana la kufanya. Inashangaza sana kwa Muislamu kulalamika kwamba anahisi uvivu kana kwamba hana Qur-aan aweze kusoma Aayah kadhaa katika Mus-haf ambapo endapo atasoma Aayah moja tu katika Qur-aan basi atapata ujira kumi kwa kila herufi moja.

Muislamu kana kwamba hana vitabu vya Dini ambavyo anaweza kusoma na kujikurubisha zaidi kwa Mola wake. Mambo muhimu sana kwa Muislamu ni mengi endapo tutayataja basi hatuwezi kuyamaliza yote, ndo maana haifai hata kid ogo Muislamu kusema kwamba anahisi uvivu au hana cha kufanya.

Waislamu wengi sana takriban asilimia hamsini tunapoteza muda wetu katika mambo ya kipuuzi na kilichochangia zaidi ni mitandao hii ya kisasa ya kiteknolojia ambayo imetengenezwa na Mayahudi kwa lengo kubwa la kumshuhulisha mwanadamu kutokufanya mambo yake yenye faida na yeye hapa duniani na huko Akhera.

Inasikitisha sana kuona Waislamu wengi tunaangamiza muda wetu mwingi katika kuangalia filamu za kipuuzi, wengine tunapoteza muda wetu mwingi kwenye kompyuta na kufanya mambo ya kipuuzi, wengine tunapoteza muda katika kuangalia video za muziki na kusikiliza nyimbo za taarabu na michezo ya kuigiza ambazo zinapoteza muda na zisizo na maadili wala faida, na wengine tunapoteza muda wetu katika mambo tofauti ambayo hayaafikiani hata kidogo na Dini yetu wala hayachangii hata kidogo katika kuueneza Uislamu duniani.

Ndugu yangu Mwislamu, tujue kwamba kuchunga muda ni katika mambo muhimu sana katika Uislamu, na ndio maana Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kaapa mahali pengi sana kwa muda katika Qur’aan kutuonyesha umuhimu wa muda. Na Allah Anapotueleza jambo fulani katika Qur’aan basi linakuwa na umuhimu na faida kubwa sana kwa Mwanaadamu.

Tukiangalia Kitabu kitukufu cha Allaah chatueleza nini kuhusu wakati, basi tutaona kwamba Allah kaapia kuhusu muda kuanzia asubuhi mpaka pale usiku unapoingia, na lengo ni kutuonyesha umuhimu na utukufu wa muda kwa Muislam.

Tukumbuke kwamba kila dakika moja inapotoweka basi hairudi nyuma na wakati wako wa maisha unazidi kupunguka. Kwa hivyo inafaa tuzingatie sana na kutumia muda wetu katika mambo mema na mazuri tu ambayo yatatukurubisha zaidi kwa Mola wetu.

Tusipoteze muda wetu kwa mambo ya kipuuzi ilihali tuko na mambo mengi ambayo yanaweza kutushughulisha yenye faida na sisi hapa Duniani na huko Akhera.

Panga muda wako vizuri kwa siku usikose kusoma Qur-aan, usikose kuongea na watoto wako na mama watoto, usikose kujifunza moja au mawili ambayo yatakusogeza zaidi kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala).

Tupunguze kazi zetu na shughuli zetu fulani na tupangilie muda fulani kudumisha malezi na tarbiyah ya Kiislamu katika majumba yetu ili tuweze kuisogeza mbele jamii yetu ya Kiislamu.

Kumbuka kwamba Malaika wa kutoa roho (Malakul Mawt) atapokuja na kuchukua roho yako, utatamani akupe angalau dakika chache ili uweze kuswali rakaa mbili.