MAWAIDHA YA KIISLAMU: Nguzo tano za Uislamu ni mfumo thabiti wa maisha kwa muumini
SIFA zote njema anastahiki Mungu Azzawajalla, swala na salamu zimwendee Mtume Mtukufu Swallallahu A’alayhi Wasallam.
Nguzo tano za Uislamu ni mfumo wa maisha ya Mwislamu.
Nazo ni ushahidi wa Imani, Swalah, utoaji wa Zakaah (kuwasaidia wenye dhiki), kufunga katika mwezi wa Ramadhaan na kuhiji Makkah mara moja maishani kwa wale wenye uwezo.
Shahada ya Imani
Ushahidi wa Imani ni kusema kwa kusadikisha, “La ilaaha illAllaah, Muhammadur Rasulullah.” Maana ya matamshi haya ni, “Hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu (Allaah), na kwamba Muhammad ni Mjumbe (Mtume) wa Mwenyezi Mungu.”
Sehemu ya kwanza, “Hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki, isipokuwa Mwenyezi Mungu,” inamaanisha kwamba hapana mwenye haki ya kuabudiwa isipokuwa Mwenyezi Mungu peke yake, na kwamba Yeye hana mshirika wala mwana.
Ushahidi huu wa Imani unaitwa Shahada, ambayo ni kanuni nyepesi ambayo inapaswa itamkwe pamoja na kusadikiwa ili mtu aweze kuingia katika Uislamu, kama ilivyoelezwa hapo juu. Ushahidi wa Imani ndio nguzo muhimu zaidi katika Uislamu.
Swala
Waislamu huswali Swala tano kila siku. Kila Swalah huchukua muda mfupi wa dakika chache tu. Swalah katika Uislamu ni mawasiliano ya moja kwa moja kati ya mja na Mwenyezi Mungu. Hakuna kishenga baina ya Mwenyezi Mungu na mfanyaji ibada.
Ndani ya Swalah, mtu hujisikia furaha, amani na faraja ndani yake, na kwamba Allaah yu radhi naye. Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Bilaal adhini, ili tufarijike nayo.)
Bilaal alikuwa mmojawapo wa Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na alikuwa mwadhini.
Swalah hufanyika wakati wa Alfajiri, Adhuhuri, Alasiri, Magharibi na ‘Ishaa. Muislam anaweza kuswali karibu mahali popote, kama vile shambani, ofisini, kiwandani au chuoni.
Kutoa Zakaah
Kila kitu ni cha Mwenyezi Mungu, hata mali zinazohifadhiwa na wanadamu kama dhamana. Maana halisi ya neno Zakaah ni zote mbili ‘kutwaharisha’ na ‘kukua.’
Maana ya kutoa Zakaah ni kutoa asilimia iliyotajwa bayana kutokana na mali fulani kwa kuyapa makundi fulani ya watu wenye dhiki. Asilimia inayopaswa kulipwa kutokana na dhahabu, fedha na pesa taslimu zenye kufikia kiasi kinacholingana na gramu 85 za dhahabu na kubaki katika miliki ya mtu kwa mwaka mmoja wa Kiislamu ni asilimia mbili unusu.
Tunavyovimiliki hutakasika kwa kutenga pembeni sehemu ndogo tu kwa ajili ya wenyedhiki, na kama vile kupogoa matawi ya mimea, huku kupunguza salio na kunatia moyo wa ukuaji mpya.
Mtu anaweza kutoa zaidi kadiri atakavyo kama Sadaka.
Mfungo wa Ramadhani
Kila mwaka katika mwezi wa Ramadhani, Waislamu hufunga tangu Alfajiri hadi kuchwa kwa jua, kwa kujizuia kula, kunywa na tendo la ndoa.
Ingawa Saumu ni yenye faida za kiafya, huchukuliwa kimsingi kuwa ni namna ya kuisafisha nafsi kiroho.
Kwa mmojawapo kujizuia dhidi ya starehe za kidunia, japo kwa muda mfupi, mfungaji hupata huruma ya kweli kwa wanaopatwa na njaa, kadhalika na kuongezeka kwa maisha yake ya kiroho.
Kuhiji Makkah
Hija ya kila mwaka Makkah ni faradhi ya kufanywa mara moja tu maishani kwa wenye uwezo wa kimwili na mali katika kuitekeleza.
Kadiri ya watu milioni mbili huenda Makkah kila mwaka kutoka kila sehemu duniani. Ingawa mara zote Makkah huwa imesheheni wageni, Hija ya mwaka hufanywa katika mwezi wa kumi na mbili katika kalenda ya Kiislamu.
Mahaji wa kiume huvaa nguo maalumu na rahisi ambayo huondosha mbali tofauti za kimatabaka na tamaduni kiasi kwamba wote huwa sawa mbele ya Mwenyezi Mungu.
Mahujaji huswali katika Msikiti wa Haram huko Makkah. Msikitini humu mna Ka’abah (jengo jeusi linaloonekana katika picha) ambalo Waislamu hulielekea wakati wakiwa katika Swalah.
Ka’abah ni mahali pa ibada ambapo Mwenyezi Mungu Aliwaamuru Mitume Ibraahiym na mwanaye, Isma’iyl waijenge.
Ibada za hija ni pamoja na kuitufu Ka’abah mara saba na kwenda mchakamchaka baina ya kilima cha Swafa na Marwa mara saba, sawa na Hajar alivyofanya wakati akitafuta maji. Kisha, Mahujaji husimama pamoja katika uwanja wa ‘Arafah na kumwomba Mwenyezi Mungu wakipendacho na kwa ajili ya maghufira, katika kile ambacho mara nyingi hufikiriwa kuwa ni onyesho la awali la Siku ya Malipo.
Mwisho wa Hijjah huweza kujulikana kwa sikukuu ya ‘Iydul-Adhw-haa, ambayo husherehekewa kwa Swalah.
Sikukuu hii na ‘Iydul-Fitwr, sherehe ya kuadhimisha mwisho wa Ramadhaan ndiyo sikukuu mbili za kila mwaka katika kalenda ya Kiislamu.