MAWAIDHA YA KIISLAMU: Rais Uhuru alionyesha heshima kubwa kusitisha hotuba yake Adhan ilipoanza

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Rais Uhuru alionyesha heshima kubwa kusitisha hotuba yake Adhan ilipoanza

Na ALI HASSAN

KWA jina la Mwenyezi Mungu mwenye kuneemesha neema kubwa na neema ndogo ndogo.

Tumejaaliwa leo hii kukutana katika uwanja wetu wa kuambizana mawili matatu kuihusu dini yetu tukufu ya Kiislamu. Uwanja ambao kwamba pia ni darsa la kuusambaza Uislamu na kumpwekesha Allah (SWT).

Kama ilivyo ada na desturi ya dini yetu hii tukufu ya Kiislamu ni kuwa tunatanguliza mambo yetu kwa kumuenzi na kumpwekesha Allah (SWT).

Hapana Mola mwengine anayestahili kuabudiwa ela ni Allah (SWT) pekee; na Mtume (SAW) ni mjumbe wake Mola wetu mmoja pekee. Kwa maana hiyo ni kuwa ni Allah (SWT) pekee ndiye Muumba wa ardhi na mbingu na vyote vilivyomo.

Leo hii ndugu yangu muumin wa dini hii tukufu ya Kiislamu tunakutana kukiwa na msiba wa ndugu zetu Watanzania kuondokewa na rais wao Hayati John Pombe Joseph Magufuli.

Kifo hiki cha aliyekuwa rais wa awamu ya tano nchini Tanzania kimesalia kuwa gumzo kubwa mno. Ni mauti ambayo yanazungumzwa sehemu mbalimbali kwa kuwa yamebadilisha nchi hiyo na kusababishwa kuandikwa kwa historia.

Mwanzo kabisa, nchi ya Tanzania sasa hivi inaongozwa na rais mwanamke, ambaye pia ni ndugu yetu Mwislamu, mama Samia Suluhu Hassan. In Shaa Allah Mola amuongoze katika majukumu yake ya uongozi. Si jambo dogo. Si lele mama. Mama Samia anao wajibu mkubwa wa kuwa rais wa kwanza mwanamke nchini Tanzania. Anahitaji maombi yetu.

Pili, kifo cha hayati Magufuli kimeutangaza mno Uislamu. Ki vipi?

Kwenye mojawapo wa hafla za kumuaga kiongozi huyo zilizoandaliwa jijini Dodoma, walialikwa viongozi wa matabaka mbalimbali wakiwemo marais na mahashumu wengineo. Rais wa Kenya, Uhuru Muigai Kenyatta alikuwa miongoni mwa viongozi waalikwa waliokuwa jijini Dodoma siku hiyo.

Angalia mipango ya Mwenye-Enzi-Mungu. Sadfa iliyoje kuwa wakati wa adhan ya swala ya dhuhr, rais Kenyatta alikuwa jukwaani akiomboleza na Watanzania. Sadfa iliyoje kuwa wakati akiwa katika simulizi zake na hotuba yake Rais Kenyatta, naye mwadhini huyo, akawa anawaita waumini kwa ajili ya ibada ya swala ya dhur.

Mipango ya Mola

Angekuwa jukwaani kiongozi mwingine siku hiyo, hatujui hali ingekuwaje. Lakini amini usimiani ndugu yangu, rais Uhuru Kenyatta akiwa katika nchi ya wenyewe – Tanzania – akisimulia, naye mwadhini ‘akamwingilia’ katikati ya hotuba yake! Naye rais Uhuru akasitisha hotuba yake hadi adhan ilipofikia kikomo! Subhannallah!

Tukio hilo punde liligeuzwa gumzo kubwa mitandaoni. Na kuzua mdahalo. Mamilioni kwa mamilioni ya watu waliokuwepo kwenye hafla hiyo, na mamilioni kwa mamilioni wengine waliokuwa wakiifuatilia kwenye runinga, mitandaoni, redioni na kwingineko kokote kule, wakabaki vinywa wazi!

Mwanzo ni kwa nini Rais akanyamaza ghafla? Na baada ya hapo, wasiokuwa Waislamu wakawa wanawahoji Waislamu na pia wenyewe kwa wenyewe: Je, adhan ni nini? Inaashiria nini? Na kwa nini rais Uhuru kuiheshimu adhan na dini ya Kiislamu kwa ujumla?

Kwa hakika hadi sasa hivi hilo ndilo gumzo. Adhan, na Uislamu; heshima ya Uhuru kwa Uislamu na maswala kama hayo. Rais Uhuru aliutangaza Uislamu ama kwa kujua au kutojua. Heshima kubwa alioupa Uislamu tunazidi kumwombea.

Mara kwa mara tumewaona wanasiasa, hasa wasiokuwa Waislamu, wakijiunga nasi katika maabadi na sherehe zetu na hata kuvishwa kanzu, kutuhutubia almradi wapate kura au kutimiza mahitaji yao.

Lakini hili la kusitisha hotuba ili adhan isikike, rais Uhuru aliutangaza mno Uislamu.

Adhan ni ibada. Sio tu jambo la kuchukuliwa vivi hivi. Ndio mwanzo wa kipindi cha swala.

Ewe ndugu yangu muumin wa dini hii tukufu ya Kiislamu, kitendo alichokifanya rais Uhuru kimetuacha na maswali mengi.

Je, angekuwa anahutubia wakati huo kiongozi Mwislamu, angesitisha hotuba yake? Ni mara ngapi tumejipitia na shughuli zetu, biashara zetu, maongezi yetu huku mwadhini anaadhini?

Ya Allah (SWT) wajaalie viongozi wengi afya, siha, nguvu na idili ya kuusambaza Uislamu ijapo kwa akali In Shaa Allah.

Ijumaa Mubarak!

alikauleni@gmail.com

You can share this post!

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Waislamu walinde umoja, undugu...

Uingereza waponda San Marino 5-0 katika mechi ya kuwinda...