MAWAIDHA YA KIISLAMU: Uaminifu ndio upeo wa imani ya mja wa Allah

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Uaminifu ndio upeo wa imani ya mja wa Allah

NA ALI HASSAN

KWA jina la Mwenyezi Mungu mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na neema ndogo ndogo.

Ni Ijumaa nyingine, siku bora na aula ambayo Mwenyezi Mungu ametujaalia kuonana, kuambizana na kukumbushana mawili matatu kuihusu dini yetu tukufu ya Kiislamu.

Awali ya yote tuchukue nafasi hii kumshukuru mno wa shukrani Muumba wetu kwa kutujaalia kuwa hai. Alhamdulillahi rabil-al-amin. Ama katika uzi uo huo twamshukuru mno Allah (SWT) kwa kutujaalia neema ya kuwa waumini wa dini ya Kiislamu.

Sawia na shukrani hizo kwa Muumba wetu, twachukua uzito wa nafasi hii kumtilia dua Mtume wetu (SAW). Atujaalie Mola sisi waumini wa dini hii tukufu ya Kiislamu tuwe waja-watiifu na wenye kufuata na kuzingatia tabia, sira, mienendo ya Mtume wetu In Shaa Allah.

Mtu akizichunga na kuzihifadhi haki za Mola wake na za wanadamu wenziwe huyo ataitwa mwaminifu mwenye amana mbele ya hadhara tukufu ya Mwenyezi Mungu na machoni mwa binadamu wenziwe.

Kuhifadhi haki za Mwenyezi Mungu hupatikana kwa kutekeleza amri na maagizo yake yote bila ya kuwa na khiyari ya kuchagua lipi utende na lipi usitende.

Umeamrishwa kuswali, basi ni lazima uswali, umeamrishwa kuwatendea wema wazazi wako basi inakulazimu kuwatendea wema.Kadhalika kuhifadhi haki za Mwenyezi Mungu ni kujiepusha na kuyaacha yote aliyokataza.

Umekatazwa ulevi, basi ni wajibu usilewe, umeharamishwa zinaa basi usizini. Kwa ujumla utakapofikia daraja ya kutenda tu lile uliloamrishwa na kuacha kila ulilokatazwa, hapo utahesabiwa mbele ya Mola wako umezihifadhi haki zake zilizokulazimu.

Ama kuhifadhi haki za binadamu, waja wa MwenyeziMungu ni pamoja na kurudisha amana za watu kwa wenyewe, zikiwa kama ulivyopewa bila kupunguza chochote wala kudai ujira.

Kutozifichua siri za watu, kutokuvunja ahadi ulizozifunga kwa uliowaahidi. Kutokumfanyia gushi/udanganyifu/utapeli mtu yeyote.

Kuvitumia viungo vyako vya mwili kwa malengo vilivyoumbiwa. Iwe kazi ya jicho lako kwenye kutizama vilivyo vya halali, ulimi utumike kusema kweli na maneno mazuri yenye nasaha. Moyo wako usimdhanie mtu kwa jambo lenye kumdhuru.

Iwapo watu watazifasiri maana hizi za kuhifadhi haki za Mwenyezi Mungu na za waja wake katika maisha yao ya kila siku, hapana shaka dunia yetu hii itakuwa ni kisiwa cha amani.Kisiwa ambacho mali na heshima za watu zina dhamana.

Mwenyezi Mungu Mtukufu anatuagiza: “Hakika Allah (SWT) anakuamrisheni kuzirudisha amana kwa wenyewe (wanaozistahiki) na mnapokubuhu baina ya watu mhukumu kwa haki [4:58]Uaminifu ni kielelezo cha imani ya mja. Haya yanathibitishwa na kauli ya Bwana Mtume – Rehma na amani zimshukie – aliposema:“Hana imani mtu asiye na amana na wala hana dini mtu asiye na ahadi” Ahmad, Ibn Hibban na Albayhaqi kutoka kwa Anas-Allah amwiye radhi.

Khiyana iliyoelezwa katika hadithi kuwa ni mojawapo ya sababu za ufakiri ni kutohifadhi haki za Mwenyezi Mungu Mtukufu na waja wake.

Hapana shaka kuwa khiyana ni miongoni mwa sifa na tabia mbaya ambayo mwislamu hapaswi kujipamba nazo. Miongoni mwa athari na sifa mbaya hizi ni: Mwenye khiyana husifika na sifa ya udanganyifu/utapeli na upungufu wa dini. Sifa hizi humuweka katika nafasi mbaya katika jamii aishimo.

Jamii humtazama kwa jicho la tahadhari kubwa, ktokana na madhara anayoweza kuwasababishia wakati wowote.

Mwenye Khiyana ana nafasi kubwa ya kutengwa na jamii, hana thamani machoni mwa wanajamii na huonekana ni mtu duni asiye na maana. Hizi ni baadhi tu ya athari za tabia hii mbaya ya khiyana. Tunasoma ndani ya Qur-ani: “Enyi mlioamini! Msimfanyie khiyana Allah (SWT) na Mtume wake (SAW) (mkaacha kufuata mliyoamrishwa) wala msikhini amana zenu (mnazoaminiana wenyewe kwa wenyewe) na hali mnajua (kuwa ni vibaya hivyo)”

Leo hii, hasa nchini mwetu, kwenye kipindi hiki cha kampeni na huku uchaguzi mkuu ukikaribia, tunawaona viongozi wakitoa kauli zenye ukinzani. Ndimi za lugha gongana! Wale, wanasiasa, waliokuwa ‘maadui; hawakai zizi moja, sasa hivi wanasifiana. Na kuonesha waziwazi jinsi uaminifu ulivyotutoka waja!Hizi ni zama za utapeli, wizi na ukosefu wa uaminifu.

Si kwamba tunawabebesha tu lawama wanasiasa, hata na sisi tunaowachagua.Ewe Mola wetu tujaalie tuwa waja-waaminifu In Shaa Allah.

Ijumaa Mubrak

alikauleni@gmail.com

  • Tags

You can share this post!

Omanyala apata saizi yake Ujerumani

PAA yajipata pabaya Jumwa akikaa ngumu

T L