Makala

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Ubora wa mwanamke na mwili wake vimo ndani ya vazi la Hijabu

November 1st, 2019 3 min read

Na HAWA ALI

MMOJA wa marafiki zangu alinisimulia tukio la kufurahisha lililomtokea Muumini mmoja wa Kiislamu.

Tukio hili lilikuwa kama ifuatavyo. Siku moja Muumini huyo alikuwa akitembea pamoja na mkewe aliyekuwa kavaa Hijabu.

Matembezi hayo yalimfikisha katika moja ya bustani zinazotembelewa na watu wa aina tofauti.

Ghafla Muumini huyo alijiwa na mtu fulani ambaye naye alikuwa na mkewe. Mke wa mtu huyu hakuwa amevaa vazi la Hijabu na hivyo basi kwa dharau na kejeli alimwambia yule Muumini, “Kwa nini umemvalisha mkeo Hijabu, kwa nini hukumuacha akatoka bila Hijabu kama jinsi alivyo mke wangu? Hijabu ina faida gani?”

Jawabu alilotoa Muumini yule lilikuwa la kushangaza na la kishujaa. Alimwambia, “Je, unafahamu tofauti ya mwanamke mwenye Hijabu na asiyekuwa na Hijabu? Bwana yule mwenye kejeli akasema, “Nini tofauti yake?” Yule Muumini akajibu kwa njia ya kuuliza, je, kuna tofauti gani baina ya teksi na gari ambalo mtu hulitumia yeye binafsi? Yaani kwa matumizi yake pekee yake?” Bwana yule akajibu akasema, “Teksi hutumiwa na kila mtu, wakati ambapo gari maalum linamhusu mwenyewe peke yake. Hii ndiyo tofauti iliyopo.” Basi yule Muumini akasema, “Hali hiyo ndiyo iliyopo baina ya mwanamke aliyevaa Hijabu na yule asiye na Hijabu.

Mwanamke asiye na Hijabu ni sawa na teksi ambayo kila mtu anaweza kuikodisha na kuitumia. Mwili wa mwanamke huyo huwa wazi na kuonesha mapambo yake na uzuri wake, na kuwafanya watu wavutike kutokana naye, jambo ambalo linaweza kusababisha kutendewa maovu, kama ambavyo mara kwa mara hali hii inavyowapata wanawake wa aina hii. Ama mwanamke aliyevaa Hijabu yeye ni bibi aliyemtukufu, ni maalum kwa ajili ya mumewe, mapambo yake na uzuri wake havionekani kwa kila mtu.

Pia watu wenye nyoyo chafu na dhaifu hawamuangalii, na uso wake na mapambo yake havikutani na macho yenye khiana, kwa kuwa amehifadhiwa ndani ya Hijabu.

Kwa hiyo utukufu wa mwanamke huyu na mwili wake vimo ndani ya hifadhi bora, pia bibi huyu hupendwa na kupendeza mbele ya mumewe na kumfanya mume kuwa na imani na mkewe, kwa sababu ya hifadhi hiyo inayomkinga kuwa na mahusiano na watu wengine kwa njia mbaya.”

Baada ya maelezo yaliyotolewa na yule Muumini wa Kiislamu, bwana yule mwenye kejeli aliona haya na akaanza kumwambia yule Muumini, “Najuta kwa kukuudhi, kwani maneno yako ni ukweli mtupu, na mifano uliyonipa ni sawa kabisa naomba samahani kwa haya niliyokutamkia na pia natubia kwa Mwenyezi Mungu kwa kitendo nilichokitenda. Kabla bwana huyu hajamaliza kujieleza mkewe alimkatiza na kusema, “Naam, naapa maneno haya aliyosema bwana huyu ni sawa na mfano aliotoa ni mzuri sana, kwani kabla ya leo nilikuwa sijasikia mawaidha kama haya. Mfano huu umeniingia moyoni nami pia natubia kwa Mwenyezi Mungu.”

Baadaye yule mume akarudia kukamilisha usemi wake akasema, “Na mimi sasa naiamini Hijabu na kuanzia leo mke wangu ataingia katika uwanja mtukufu kwa kuvaa Hijabu. Kamwe sikubali mke wangu atoke bila Hijabu, kwani ndilo vazi la amani na imani. Nafsi yangu haipendi kabisa kumuona mke wangu akidhihiri mbele za watu kama kwamba yeye ni kwa ajili ya kila mtu.”

Kwa kuvaa Hijabu, mwanamke huyu atakuwa amepata radhi za Mola wake na kupata utukufu wa watu wa peponi. Kwa vazi hili mwanamke huyu huvutia mvuto wa ucha Mungu na heshima. Pia dalili za utulivu hujitokeza kwa mwanamke huyu na dhana njema kwake hutawala fikra za kila amuonaye. Amtazamapo mwenye kumtazama, huwa ni shida kutambua, je, mwanamke huyu ni msichana au ni mtu mzima? Sura yake ikoje nzuri au la? Hutatizika wanaomuangalia. Matokeo yake watu humuangalia kwa jicho la heshima, hakuna awezaye kumkabili kwa maneno machafu au maudhi, kwani anafahamu wazi kwamba mwanamke huyo ameshikamana na dini yake na anaheshimu utu wake. Isitoshe mwanamke kama huyu huwa amejitenga na matendo ya aibu na kujiepusha na wanawake wasio na sitara, na kwa ajili hiyo hayuko tayari kuidhalilisha nafsi yake.

Huo ndiyo mfano wa mwanamke mmoja na namna alivyojiweka katika jamii yake.

Kwa upande wa yule mwanamke wa pili, ni yule asiyejali kujisitiri uso wake amevua vazi la la stara, hana aibu wala haya. Kwa maana hiyo ameing’oa imani yake, kwa sababu Mtume anasema: “Mtu kuwa na haya ni sehemu ya imani, na mtu asiye na haya hana imani.”

Kwa mwenendo wake mwanamke huyu, huwa ni mpinzani mkubwa wa muongozo wa Qur’an na huwa anajidhalilisha kwa kuonyesha mapambo yake, kama walivyokuwa wakionyesha mapambo yao wanawake wa zama za kijahiliya kabla ya kuja Uislamu.

Isitoshe kwa mwanamke huyu, hali aliyo nayo huwa amejifananisha na wanawake wa Kiyahudi na Kinaswara, na huwa yuko mbali na heshima yake na utu wake. Kutokana na kuudhihirisha mwili wake na uso wke na mikono yake, pia kifua chake na sehemu nyingine katika maumbile ya kike. Watu waovu na wenye tamaa huyaona wazi wazi maumbile yake na hapo tayari anakuwa mfano wa bidhaa zilizotandazwa sokoni, kwani kila mtu ana uhuru wa kuziangalia bila mipaka.

Matokeo ya uovu wa mwanamke huyu, ni kupata usumbufu toka kwa wahuni ambapo hatimaye wanaweza kumtendea matendo machafu yanayoweza kumharibia thwahara yake.