Makala

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Uislamu ni dini ambayo inahimiza amani, upendo na uvumilivu

September 6th, 2019 3 min read

Na HAWA ALI

SIFA zote njema anastahiki Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na mwenye kurehemu.

Sala na salamu zimthibitikie Mtume wetu Muhammad Swallallahu Alayhi Wasallam, maswahaba wake watukufu na watangu wema hadi siku ya Kiyaamah.

Neno Uislamu linamaanisha amani kwa Kiarabu. Uislamu ni dini iliyoteremshwa ili kumwakilisha mtu pamoja na maisha yaliyojaa utulivu na amani ambayo yana huruma isiyo na mwisho ya Allah iko waziwazi. Allah anawaita watu kuja katika maadili ya Uisilamu kuwa ndio kigezo ambacho huruma, uvumilivu na amani vinaweza kufanyiwa kazi. Yafuatayo yanaelezwa katika aya 208 ya sura al-Baqara:

“Enyi mlio amini! Ingieni katika Uislamu kwa ukamilifu, wala msifuate nyayo za She’tani; hakika yeye kwenu ni adui aliye wazi.”

Kama inavyoonekana katika aya, Allah anaeleza kuwa usalama wa watu unaweza kuhakikishwa tu kupitia kuukubali Uisilamu na kutekeleza kwa vitendo maadili ya Quran.

Uisilamu unaulinda uhuru wa kutafakari na uvumilivu

Uislamu, ambayo ni dini inayoeleza na kuhakikisha waziwazi uhuru wa kutafakari na maisha, imetoa maamrisho yanayozuia na kukataza kuwekana roho juu, migogoro kati ya watu, kusemana na hata kuwadhania watu vibaya.

Sio tu kutishia na matumizi ya nguvu, Uisilamu unakataza kuweka hata shinikizo dogo kwenye fikra za watu.

“Hapana kulazimisha katika Dini. Kwani Uwongofu umekwisha pambanuka na upotofu.” (al-Baqara, 2/256)

“Wewe si mwenye kuwatawalia.” (al-Ghashiya, 88/22)

Ni kinyume na maumbile na uhalisia wa Uislamu kuwateza nguvu watu ili waamini katika dini au kufanya ibada. Kwa kuwa, Uislamu umeweka utashi huru na ridhaa makini kuwa ndio sharti la imani. Bila ya shaka, Waislamu wanaweza kuonya na kuhamasishana hivyo wanaweza kutekeleza kwa vitendo sifa za kimaadili zilizofafanuliwa ndani ya Quran. Hata hivyo, hawawezi kutezana nguvu kuhusiana na hilo. Sio sawa kupendekeza vipaumbele fulani vya kidunia ili kumfanya mtu fulani afanye ibada.

Fikiria kuhusu kigezo cha jumuia kilicho kinyume cha mtindo wa hilo. Mathalani, jaalia kuwa watu wanatezwa nguvu kuabudu. Jumuia ya namna hiyo iko kinyume kabisa na Uisilamu. Kwa kuwa, imani na ibada vinakuwa na thamani vinapotekelezwa kwa ajili ya Allah. Ikiwa mfumo wa utawala utawalazimisha watu kuamini na kuabudu, watu watakuwa ni washika dini kwa sababu ya kuuogopa mfumo-tawala.

Kilichokuwa na thamani kwa upande wa dini ni kutekeleza dini kwa vitendo kwa ajili ya Allah katika mazingira huru kabisa.

Allah ameharamisha kuua watu wasio na hatia Kwa mujibu wa Quran, kumuua mtu asiye na hatia ni moja ya madhambi makubwa mno:

“…aliye muuwa mtu bila ya yeye kuua, au kufanya uchafuzi katika nchi, basi ni kama amewauwa watu wote. Na mwenye kumuokoa mtu na mauti ni kama amewaokoa watu wote. Na hakika waliwajia Mitume wetu na hoja zilizo wazi. Kisha wengi katika wao baada ya haya wakawa waharibifu katika nchi.” (al-Maida, 5/32)

“Na wale wasio mwomba mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu, wala hawaui nafsi aliyoiharamisha Mwenyezi Mungu isipo kuwa kwa haki, wala hawazini – na atakaye fanya hayo atapata madhara,” (al-Furqan, 25/68)

Kama inavyoonekanwa katika aya hapo juu, wale wanaoua watu wasiokuwa na hatia wanaonywa na adhabu kali. Allah anaeleza kuwa kumuua mtu mmoja ni uhalifu mkubwa mno kama kuua watu wote. Haiwezekani kwa mtu anayetii mipaka iliyowekwa na Allah kumdhuru hata mmoja achilia mbali kuua maelfu ya watu wasio na hatia.

Kukwepa haki

Wale wanaodhani kwamba wanaweza kuikwepa haki na kunusurika nayo hawatoweza kukwepa kisasi mbele ya Allah.

Kwa hivyo, waumini wanaojua kwamba watalipiziwa mbele ya Allah baada ya kifo wanatenda mambo kwa uangalifu mno ili kutii mipaka iliyowekwa na Allah. Allah anawaamuru waumini kuwa na huruma.

Maadili ya Mwislamu yanafafanuliwa kama ifuatavyo katika aya:

“Tena awe miongoni mwa walioamini na wakausiana kusubiri na wakausiana kuhurumiana. Hao ndio watu wa kheri wa kuliani.” (al-Balad, 90/17-18)

Moja ya sifa muhimu mno za maadili yaliyoteremshwa na Allah kwa waja Wake ili wapate wokovu Siku ya Kiama, rehema Zake na Pepo ni “kuamrishana subira”. Uisilamu, unaoelezwa katika Quran, una muundo wa kisasa, wenye kuelimisha na wa kimaendeleo. Mwisilamu wa kweli anayo haiba ya amani, uvumilivu, kidemokrasia, kitamaduni, utambuzi/usomi, uaminifu, jicho la sanaa na sayansi na ustaarabu.

Mwisilamu aliyelelewa na maadili ya juu yaliyotajwa na Quran anatangamana na kila mtu kwa upendo unaotumainiwa na Uisilamu.