Makala

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Ya Rabi tunusuru na janga hili la mafuriko katika maeneo mbalimbali ya nchi

November 29th, 2019 3 min read

Na ALI HASSAN

KWA jina la Mwenyezi Mungu mwenye kuneemesha neema kubwakubwa na neema ndogondogo.

Leo hii tumejaaliwa kwa kudura zake Maulana kukutana katika siku hii tukufu ili kukumbushana mawili matatu kuihusu dini yetu tukufu ya Kiislamu.

Awali ya yote ndugu yangu muumin Mwislamu twatanguliza makala yetu kama ilivyo ada kwa kumshukuru mno Mola wetu kwa kutujaalia sio tu kuwa hai na wenye nguvu za kutekeleza ibada na kujaaliwa kuwa Waislamu, lakini kwa sababu ya yeye Mola kuwa ndiye pekee anayepaswa kuabudiwa.

Hili lina maana kuwa hapana mwingine anayepaswa kuabudiwa ela Mola wetu mmoja pekee mwenye kuumba ardhi na mbingu na vyote vilivyomo. Yaani hakipumui kiumbe ila ni kwa mapenzi yake Maulana.

Hakizaliwi kiumbe ela ni kwa mapenzi yake Muumba wetu. Hakiondoka duniani kwa maana ya kufariki dunia kiumbe ela ni kwa kudura na mapenzi yake Allah (SWT).

Ama baada ya kumsifia sana Mola wetu na kummininia utukufu wote huo, twachukua sawia nafasi hii sisi waumini wa dini yetu tukufu ya Kiislamu kumtilia dua na kumtakia maombi na kheri Mtume wetu (SAW).

Leo hii ndugu yangu tupo katika kipindi kigumu na pia kipindi cha baraka na neema. Baraka na neema kama tulivyosema majuzi kwenye makala yaya haya kuhusu dua maalum inapokuwa ikinya mvua.

“Ewe Mwenyezi Mungu, tuokoe kwa kututeremshia mvua, Ewe Mwenyezi Mungu, tuokoe kwa kututeremshia mvua”

“Ewe Mwenyezi Mungu, tuokoe kwa kututeremshia mvua. Ewe Mwenyezi Mungu wanyeshelezee waja wako, na wanyama wako, na eneza rehema zako, na fufua nchi yako iliyokufa.

Kutoka kwa Bibi Aisha R.A.A.H. kasema, “Mtume S.A.W. anapoona mvua (inanyesha) alikuwa akisema:

Allahumma ij`alhu sayyiban hanian.

Maana yake, “Ewe Mwenyezi Mungu ijaalie iwe mvua kubwa nzuri (yenye kheri)”.

Ama dua zetu zimejibiwa. Zanya mvua. Alhamdulillahi!

Hata hivyo, upo mtihani mwingine. Nao ni mtihani wa mvua kunya kupita kiasi.

Ni kipindi kigumu cha msiba ambapo waja wameaga dunia kutokana na mafuriko. Hadi tunapoyaandaa makala haya, waja wapatao zaidi ya hamsini walikuwa wametangulia mbele za haki. Kuondoka duniani kwa wenzetu hawa kunatuachia msiba wa majonzi.

Ya Rabi tunusuru na janga hili la mafuriko.

Aidha, ni mkasa na kisa kwa jamaa ambao wameondokewa na jamaa zao huku nao wakiwa wanaishi pasina makao. Nyumba zao, mifugo yao, maboma yao, mashamba yao, mazao yao, riziki zao zimesombwa na mvua hizi kubwa ambazo zanya kwa sasa.

Ewe Mola twakuomba na kukulilia utupe nguvu na mwisho mwema. Utupe nguvu wote ambao wameathirika kwa njia moja ama nyingine kutokana na msiba huu.

Majonzi haya yameishia pia kwenye kusombwa kwa muundo mbinu. Madaraja yamesombwa. Uchukuzi umekuwa mtihani. Waathirika hawafikiwa katu. Yaani hali ni ngumu sana waja kwa sasa.

Sasa hivi waathirika wamelazwa katika hospitali mbalimbali. Hali zao taabani. Twaomba Mola awajaalie afya. Na huko kunakohitajika msaada wowote ule kwa hali na mali tuchangie kwa moyo mkunjufu maana waambiwa kuwa kutoa ni moyo usambe ni utajiri.

Hata huko majumbani kwetu sasa hivi ni matope ni vinamasi. Ndio hapo basi twaomba watumizi wa magari kuwa makini sana barabarani tusiwafanyie madharau watumizi wa barabara wanaotumia miguu. Utu tu.

Hakuna kimbilio na tegemeo letu sisi waja isipokuwa Mola Moliwa mjuzi wa kila jambo.

Maisha kwa sasa ni hekaheka. Mabilioni ya senti yataishia kwenye ujenzi mpya wa muundo mbinu ambao umeharibika vibaya vibaya!

Ni jambo la kuhuzunisha kuwaona wenzetu wakisombwa na maji. Rasilmali zikifyekwa na maji. Maji ambayo ni uhai. Huku hayo yakijiri nayo mifereji yetu haina hata tone la maji. Maji yanapotea bure.

Badala ya kuwa faida ya uwekezaji, sisi waja tunashuhudia maji yakijimwagikia shelabela.

Ya Rabi tupe nguvu na ujuzi wa kuyatumia maji vema. Ewe Mola wetu tujaalie ziwe mvua za kheri. Ziwe mvua za baraka In shaa Allah.

 

Ijumaa Kareem!

 

[email protected]